January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB Mshiko Fasta kuwanufaisha wakulima

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imekuja suluhisho maalum ya kuwakopesha mitaji kwa wateja wake unaojulikana kwa jina la ‘NMB Mshiko Fasta’ ambapo unawawezesha wateja wao kupata mikopo midogo midogo wa hadi 500,000 ukiwa na NMB Mkononi kupitia simu yako tu.

Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Ndg. Isaac Masusu aliyasema hayo kwenye maonyesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Alitoa taarifa hiyo wakati Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Tulia Ackson alipotembelea banda la benki hiyo kwa lengo la kujua huduma mbalimbali ambazo zinatolewa kwa watanzania hasa wakulima.

Masusu alisema mfumo huo unawawezesha wakulima kukopa mpaka Sh. 500,000 bila dhamana yoyote kwa kutumia simu zao na kwamba hata wanaotumia simu za kawaida ambazo sio simu janja wanapata huduma hiyo wakiwa sehemu yoyote na kuongezea kuwa itawawezesha wakulima kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

“Kwa wale wakulima ambao wanalima ekari moja ama mbili hapa ndio mahali pake, kinachotakiwa ni mteja awe na akaunti kwenye benki yetu na awe anaitumia, hii itatufanya tumtambue na tuweze kumkopesha,” alisema Masusu.

Aliongezea kuwa mfumo huo pia unawaunganisha wakulima na wajasiliamali kwenye kituo kimoja cha kuwahudumia na kwamba watakuwa wanapata huduma zote kwa njia ya simu.

Alisema hata mfumo wa ununuzi wa pembejeo za kilimo kwa njia ya ruzuku ikiwemo mbolea utafanya kazi kwa mfumo huo na kwamba utawasaidia wakulima kukabiliana na baadhi ya matatizo ikiwemo ukosefu wa mitaji.

Dk. Tulia aliipongeza Benki ya NMB kwa kubuni mfumo huo akisisitiza kuwa utawasaidia wananchi kukabiliana na baadhi ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwakabili kwenye shughuli zao za uzalishaji hasa ukosefu wa mitaji na kuwataka wananchi wanaokopa fedha kwenye benki hiyo wahakikishe wanazitumia kwa malengo husika na kurejesha kwa wakati ili na wengine wanufaike.

Bado wapo kwenye maonesho ya Nane Nane jijini Mbeya, tembelea banda lao ili uweze kunufaika na huduma zao za kibenki.

Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki ya NMB, Isaac Masusu akimweleza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson namna ambavyo wakulima wananufaika na mikopo nafuu ya NMB alipotembelea banda lao katika wa maonesho ya wakulima Nane Nane