November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB MastaBata Kote Kote yazidi kupasua anga

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampeni ya NMB MastaBata ‘Kote Kote,’ inayoendeshwa na Benki ya NMB, imezidi kupasua anga baada ya zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 10.5 kutolewa kwa washindi 76 jana, hivyo kufanya jumla kuu ya zawadi kufikia zaidi ya Sh. Mil. 96.5 kati ya Sh. Mil. 350 zilizotengwa.

Washindi 76 walipatikana wakati wa droo ya tano iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, ambako pia washindi wa pikipiki wa droo ya nne na washindi wa safari ya Zanzibar iliyolipiwa kila kitu na NMB, walikabidhiwa zawadi na tiketi zao.

Katika droo hio iliyochezeshwa chini ya Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Salim Bugufi, ilishuhudiwa David Kaaya akiibuka mshindi wa bodaboda yenye thamani ya Sh. Mil. 3, huku washindi wengine 75 wakijinyakulia Sh. 100,000 kila mmoja.

Katika hafla hiyo, Elihuruma Minja na Grace Mponeja walikabidhiwa tiketi za safari ya kwenda Zanzibar (wao na wenza wao), ambako watahudhuria tamasha la Zanzibar Full Moon Party, huku Hamza Hamood akikabidhiwa pikipiki aliyoshinda katika droo iliyopita.

Akizungumza kabla ya droo hiyo, Meneja Mwandamizi Biashara za Kadi NMB, David Ngusa, alisema tayari zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 86 zilishatolewa kwa washindi mbalimbali waliopatikana katika wiki nne za kampeni hiyo inayofanyika kwa msimu wa nne sasa.

“Ni kampeni inayohamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu ‘cashless,’ ambayo ni salama na nafuu zaidi, ambako tumetenga zaidi ya Sh. Mil. 350 kuwazawadia wateja wetu wanaotumia kadi za NMB mastercard kwa kutumia POS, Online au Lipa Mkononi (QR Code).”

“Kila wiki tunakabidhi Sh. Mil. 7.5 kwa washindi 75, huku tukitoa pikipiki moja. Lakini pia tuna droo za mwezi, tunakowazawadia Sh. Mil 1 washindi 49, sambamba na bodaboda mbili, na droo ya fainali itazawadia safari za Dubai kwa washindi saba na wenza wao kwa siku nne,” alisema Ngusa.

Kwa upande wake, Bugufi alibainisha kuwa usimamizi wa droo za NMB MastaBata uko chini ya GBT, ambayo ni taasisi tanzu ya Serikali yenye jukumu hilo, hivyo kuwataka Watanzania kufanya matumizi yasiyo ya pesa taslimu ili kuwania zawadi mbalimbali za kampeni hiyo.

Baada ya kukabidhiwa tiketi zao za kwenda Zanzibar kuhudhuria Tamasha la Full Moon Party linalofanyika katika fukwe za Kendwa Rocks, Elihuruma na Grace waliishukuru NMB kwa fursa adhimu ya utalii wa ndani waliyoipata mwishoni mwa mwaka wao na wenza wao.

Meneja Mwandamizi Biashara za Kadi Benki ya NMB, David Ngusa (kulia) na Meneja wa NMB Tawi la Bank House, Seka Urio (kushoto) wakimkabidhi tiketi ya kuhudhuria tamasha la Fullmoon Party visiwani Zanzibar, Elihuruma Minja (katikati), mshindi wa droo ya nne ya Kampeni ya NMB MastaBata ‘Kote Kote’ inayohamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu.