July 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB: Mafanikio Yanga ni matokeo ya kuzitumia ‘4R’ za Rais Samia

Na Mwandishi wetu ,Timesmajira

BENKI ya NMB imedhamini Uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Klabu ya Yanga, huku Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake BiRuth Zaipuna akisema mafanikio mfululizo ya timu hiyo ni matokeo ya ubunifu wa uongozi kuichakata na kuigeuzia michezoni Falsafa ya R4 ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Falsafa ya R4 au ‘4R’ imeasisiwa na kutumiwa na Rais Samia kama dira ya utekelezaji wa majukumu yake katika kuyafikia mafanikio endelevu ya taifa, ambapo Zaipuna anaamini uongozi wa Yanga umezichakata 4R hizo na hatimaye kupata mafanikio ya kupigiwa mfano ndani na nje ya uwanja

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, aliyemwakilisha Rais Samia,  Zaipuna aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa mchango na mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo michezo ambako Taifa limefanya vizuri.

“Nadhani katika kipindi hiki, kama taifa tumeshuhudia mafanikio makubwa katika soka, ambako Taifa Stars ilifuzu tena Fainali za Afrika (AFCON 2023), na kuwa moja ya timu chache kutoka Ukanda wa CECAFA, ngazi ya vilabu nako, tumeshuhudia klabu zetu zikijenga heshima kubwa.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, unapozungumzia Falsafa ile ya 4R ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ile Reconciliation yaani Maridhiano, Resilience – Ustahimilivu au Utulivu, Reforms yaani Mageuzi au Mabadiliko na Rebuilding – Kujenga Upya, nadhani Yanga ni mfano bora wa namna ya kuzitumia hizi 4R.

“Matumizi ya falsafa hiyo yamefanikiwa kuijenga Yanga kuwa klabu bora, imara ndani na nje ya uwanja, klabu inayoongozwa kwa misingi ya Utawala Bora na umoja baina ya wanachama, mashabiki, uongozi na wadau wa soka nchini Tanzania,” alisema Bi. Zaipuna na kushangiliwa mno.

Akifafanua,  Zaipuna alisema: “Yanga hii ya leo, imepitia Maridhiano yaliyoleta umoja huu tunaouona leo, lakini pia Yanga hii imepitia nyakati ngumu zilizohitaji Ustahimilivu wa changamoto mbalimbali, wakitambua kuwa ni sehemu ya maisha ya binadamu au taasisi tunazoziongoza.

“Pia, Yanga hii imepitia Mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kiutawala, kiuendeshaji na hata kiuwekezaji kwa ustawi wa klabu hii, ambayo Imejijenga Upya na inaendelea kujijennga kuwa taasisi ya michezo ya kuigwa Tanzania na Afrika Mashariki, ikivutia nyota wakubwa Afrika.

“Kwa muktadha huo, nitumie nafasi hii kumpongeza kila mmoja ndani ya Yanga kwa maafanikio iliyoyapata miaka hii, ambayo yanaliletea taifa heshima,” alisisitiza Bi. Zaipuna mbele ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Zaipuna aliishukuru Yanga kwa kuendelea kushirikiana na NMB katika nyanja mbalimbali, na kwamba udhamini wao katika uzinduzi huo wa kitabu cha historia yao sio mwanzo wa mashirikiano baina ya pande hizo mbili zenye rekodi kubwa za mafanikio kama taasisi.

“Ushirikiano wa NMB na Yanga umeanza muda sasa, mtakumbuka mwaka jana tulianza ushirikiano huu kwa kusaini makubaliano ya mchakato wa kurahisisha usajili wa wanachama na mashabiki wa klabu hii kongwe kwa kutumia mtandao wa matawi yetu kote nchini.