December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Na Penina Malundo,DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amesema kuwa chama cha NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Doyo alisisitiza kuwa chama cha NLD kimefanya tathmini ya kina kabla ya kushiriki katika uchaguzi huu, na kimejiridhisha kuwa kitafanya vyema katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji.

Ameyasema hayo jana Mkoani Tanga,wakati akiongea na waandishi wa habari amesema kuwa chama hicho kimesimamisha wagombea zaidi ya 600 katika maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo idadi ya wagombea jumla ni 700, ikijumuisha wagombea wa nafasi mbalimbali za ujumbe.

Doyo ameipongeza Tamisemi kwa usimamizi bora wa zoezi la undikishaji na urejeshaji wa fomu, akibainisha kuwa mwaka huu zoezi limeenda vizuri ikilinganishwa na mwaka 2020. Pia Doyo amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa “4R” za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha demokrasia, huku alisisitiza kuwa ameziona “4R” za Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo katika maandalizi ya uchaguzi huu wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji.

Chama cha NLD kina matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, huku kikitarajia kupata ushindi katika baadhi ya maeneo katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa.