Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MWENYEITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora Said Samwel Nkumba amewataka Viongozi wa Chama na Serikali kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha miradi ya wananchi inatekelezwa ipasavyo.
Ametoa rai hiyo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Mkoani hapa ambapo alibainisha kuwa Chama kinajivunia kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa haya yanayofanyika sasa ni utekelezaji ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo imebainisha wazi mambo yote yatakayofanywa na serikali yake katika sekta zote ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Nkumba amefafanua kuwa serikali imeendelea kuleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali, hivyo Viongozi wa Chama na Serikali wanapaswa kushikamana ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo.
‘CCM Mkoa wa Tabora tunampongeza sana Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya ya kuwaletea maendeleo wananchi’, amesema.
Amewataka wanaCCM kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano kama ilivyo kawaida yao kuelekea kwenye Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha chama hicho kinaendelea kufanya vizuri katika chaguzi zote.
Said Nkumba alisisitiza kuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu Chama Cha Mapinduzi kitaweka wagombea wanaokubalika kwa wananchi ambao watasimamia kwa dhati maendeleo ya jamii.
Ameonya kuwa Chama hakitamvumilia mgombea yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo na kusisistiza kuwa watakaotoa rushwa hawatapata nafasi.
Amewataka wale wote watakaogombea kupitia Chama hicho kujiandaa vizuri na sio kuandaa fedha za kutoa rushwa huku akisisitiza kuwa hatawafumbia macho wagombea wa namna hiyo.
Mwenyekiti ameongeza kuwa huu ni wakati wa wanaCCM kuweka tofauti zao pembeni ili kukipigania chama, aliwataka viongozi wa chama kuanzia ngazi za chini kuwasamehe waliowasimamisha ili waunganishe nguvu zao pamoja.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya