November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nkuba aahidi kuimarisha miundombinu TLS

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Sweetbert Nkuba, ambaye ni miongoni mwa wagombea sita wa nafasi ya urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), moja ya sera zake ni uimarishaji wa miundombinu ya kisheria na kiteknolojia ndani ya TLS ili kuwezesha huduma bora kwa wanachama na jamii kwa ujumla.

Hiyo ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria na kuboresha ofisi za TLS katika mikoa mbalimbali kwa vifaa vya kisasa na miundombinu bora.

Nkuba alisisitiza mwishoni mwa wiki kuhusu mafunzo endelevu kwa wanachama wa TLS ili kuhakikisha kuwa wanasheria wana ujuzi wa kisasa na uwezo wa kushindana kimataifa na kwamba hiyo itajumuisha kuanzisha programu za mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria mpya na mabadiliko ya sheria na kushirikiana na taasisi za kimataifa kwa mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Kuhusu ushawishi na utetezi, Nkuba alisema sera yake ni kuhakikisha  TLS inakuwa na sauti yenye nguvu katika masuala ya kitaifa na kimataifa yanayohusu sheria na haki na kwamba  itajumuisha kuanzisha mikakati ya ushawishi kwa serikali na bunge ili kuboresha mfumo wa sheria nchini na kutoa msaada wa kisheria kwa jamii, hususan makundi yenye uhitaji maalum.

Kuhusu uwajibikaji alisema atalenga kusimamia kwa uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote za TLS ili kujenga imani kwa wanachama na wadau wengine na kwamba hilo litajumuisha kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani na nje ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za TLS na kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wanachama kuhusu shughuli na matumizi ya fedha za TLS.

Katika kujenga uhusiano Imara Nkuba alisema atahakikisha anajenga na kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, ikiwemo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na taasisi za kimataifa na kuanzisha na kudumisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa ya kisheria kwa manufaa ya wanachama wa TLS pamoja na kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika kutoa elimu ya sheria na mafunzo ya vitendo.

Kuhusu  Kukuza Uongozi na Ushirikishwaji alisema  atahakikisha wanachama wa TLS wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi wa chama na kwamba hiyo itajumuisha kuanzisha mifumo ya ushirikishwaji wa wanachama katika maamuzi muhimu na kutoa fursa kwa wanachama wote, hususan wanawake na vijana, kushiriki katika nafasi za uongozi.

Kwa sera na mtazamo huo, Sweetbert Nkuba alisem anaamini ataweza kuiboresha TLS na kuifanya kuwa chama imara na chenye ushawishi mkubwa katika sekta ya sheria nchini Tanzania.