November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Njeza awahakikishia wananchi kuendelea kutatuliwa changamoto na serikali

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya vijijini ,Oran  Njeza amesema kuwa serikali itaendelea kutatua  kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jimbo  hilo kama ambavyo baadhi zimeendelea kushughulikiwa kwa wakati.

Mbunge Njeza amesema hayo leo,Julai 12,2024 akiwa katika vijiji vya Izumbwe,na Iwiji  kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo barabara,maji na umeme na kusema serikali inaendelea na jitihada za kutatua changamoto za wananchi.

Akisoma risala Mbele ya Mbunge Njeza,  Ofisa  mtendaji wa kijiji cha Izumbwe,Kambona Mwahalende ameomba  kutatuliwa kero zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji safi na ubovu wa barabara.

Wananchi hao pia wakitoa kero zao kwa Mbunge wa Mbeya vijijini, wamesema barabara bado ni tatizo katani kwao ikiwemo barabara ya Sayuma hadi Ileya B kisha kutokea kijiji jirani cha Mwakasita ambayo wameomba iangaliwe licha ya kwamba daraja katika eneo lililokuwa korofi tayari lilishajengwa.

Hata hivyo wananchi hao wameomba kumaliziwa usambazaji wa nishati ya umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havijafikiwa ikiwemo shuleni ili wanafunzi wajisomee vizuri.

Akijibu hoja za miundombinu ya barabara Mhandisi, Arcad Tesha ambaye ni Kaimu meneja wa Wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA wilaya ya Mbeya amesema barabara inayolalamikiwa kutoka Sayuma kwenda hadi kijiji jirani cha Mwakasita haitambulikani hivyo wataifuatilia ili kuiingiza kwenye mpango wa bajeti.

Naye Mhandisi wa maji kutoka Wakala wa  Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) wilaya ya Mbeya ,Evetha Nzogela kwa niaba ya meneja wa RUWASA wilaya amesema wadau ambao ni shirika lisilo la kiserikali CRS limejitoa kujenga mradi wa maji katika moja ya vijiji vitatu vya kata ya Iwiji na endapo kijiji cha Izumbwe hakitanufaika RUWASA itahakikisha inakikumbuka kijiji hicho ili kumtua mama ndoo kichwani kwa kutafuta chanzo cha maji ili kujenga mradi kwa maslahi ya wananchi hao.

Mhandisi Nzogela amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki wakati wahisani hao wakiandaa mazingira ya kujenga mradi katani humo.