Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Charles Njama amesema atashirikiana na madiwani wenzake kuona wanaleta maendeleo kwa makundi yote ya wananchi.
Na katika kuleta maendeleo hayo, atahakikisha makundi ya mamalishe, babalishe, wanawake wauza mahindi, mbogamboga, bodaboda, bajaj, maguta, na ujasiriamali mwingine, wanafanya shughuli zao za kujipatia kipato kwa kuwaboreshea mazingira na kupata mitaji isiyokuwa na riba ikiwemo fedha za asilimia 10 kutoka halmashauri.

Ameyasema hayo Septemba 11, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Kampeni Jimbo la Korogwe Mjini uliofanyika Uwanja wa Sokoni mjini Korogwe, ambapo amesema changamoto kwake ni fursa, hivyo anataka kuona wananchi wa jimbo hilo wanapata maendeleo bila kuogopa changamoto zilizopo mbele yao.
Njama amesema akipata ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini atakwenda bungeni akiwa na vipaumbele vilivyobainishwa na wananchi wenyewe, na yeye atakuwa sauti ya wananchi kuona anawajibika kadiri atakavyojaliwa na Mungu, lakini na jitihada zake kuona wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini wanapata maendeleo.

“Mimi ni muumini wa utu. Ninaamini utu na kufanya kazi kama nguzo imara ya kwenda kutafuta maendeleo. Ninaamini katika uwajibikaji, nalo nitakwenda kulifanya kwa niaba yenu. Mimi si chochote wala lolote miongoni mwa ninyi mliopo hapa, bali ni neema ya Mungu tu sababu ni mmoja tu anaeweza kutuwakilisha sisi sote, na naamini ninyi mmenichagua kama kipaza sauti chenu, na kazi yangu nitakayokwenda kuifanya ni ile mtakayonituma ninyi.Kama muwakilishi wenu, ninalo jukumu na nitalifanya kwa uaminifu, la kuwasikiliza, kupokea, kuwakilisha na kurudisha majibu.

“Hiyo kazi nitaifanya kwa vile nimeacha mengi kwa ajili ya hilo, kwa ajili ya watu wa Korogwe, na ninaomba Mungu akaniongoze. Ninaamini sana katika ushirikishwaji, na siamini katika maamuzi ya mtu mmoja, hivyo kila mmoja wenu anayo nafasi, na tutaitumia vizuri kuhakikisha dhana ya ushirikishwaji inatendeka ipasavyo. Ninaamini sana katika ukweli na uwazi, nami nitajitahidi kuwa mkweli kwenu kadiri inavyowezekana. Nitajitahidi kuwa muwazi kwenu kadiri inavyowezekana, nitajitahidi kuifanya halmashauri yangu kuwa wa wazi kwenu kadiri inavyowezekana. Nitajitahidi kuwafanya viongozi wenzangu tuwe pamoja na wawajibikaji kwa wananchi waliotupa dhamana ambao ni watu wa Korogwe” amesema Njama.
Njama ambaye kwa taaluma ni Mhasibu, amesema anaamini ataweza kusaidia changamoto kuwq fursa badala ya kuwa kero, hivyo kikubwa ni kuona anapata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Serikali na wananchi wote wa Korogwe.

“Changamoto zetu ni fursa, na hakuna changamoto inayoweza kutuzuia kusonga mbele tukiamua kwa pamoja. Nimebahatika kukaa na vikundi mbalimbali, nimekaa na akina Mamalishe na babalishe, nimekaa na vikundi vya bodaboda, bajaj na maguta. Nimepita sokoni na kukutana na wanawake wanaouza mahindi na mbogamboga, makundi hayo ni muhimu sana katika historia ya maisha yangu, nami nitaungana nayo kwa uwezo wangu wote, kuhakikisha ninaacha mchango utakaoweza kuishi kwenye maisha ya watu kwa miaka ijayo… nimekuja kwa sababu hiyo.
“Tuombe Mungu atupe afya, tuombe ulinzi, tuwe na amani na mshikamano, tuepuke majungu ili tukaijenge Korogwe yetu. Mimi ni Mbunge wenu Mungu akipenda, na siyo Mbunge wa mtu mmoja, hivyo nitatoa nafasi kwa kila mmoja ili twende tukajenge Korogwe yetu kwa umoja wetu” amesema Njama.

Njama amesema, pamoja na Ilani kusheheni mambo mengi ikiwemo kuwasaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba kupitia halmashauri, lakini kuna haja ya kupata makampuni yatakayotokana na makundi ya vijana ili vijana hao wapate kipato, na jambo hilo litakuwa la mfano kwa maeneo mengine ya nchi, na wao wataiga kupitia Jimbo la Korogwe Mjini.
Naye, Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini, Thobias Nungu, ambaye pia aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa na chama kugombea ubunge Jimbo la Korogwe Mjini, aliwaomba wananchi kumchagua mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vile amefanya mengi kwenye jimbo hilo. Lakini pia wamchague CPA Njama, na madiwani 11 wa jimbo hilo.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako