Na Mwandishi Wetu
CHUO cha Taifa Usafirishaji (NIT), kipo mbioni kuanzisha kitengo cha mafunzo ya usafiri wa reli mkoani Tabora kwa ufadhili wa Serikali ili kuendana na kasi ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika usafiri wa reli.
Aidha, chuo hicho kati ya Desemba mwaka huu na Januari mwakani kinatarajia kupokea ndege mbili za mafunzo ya upairoti hapa nchi na kitakabidhiwa rasmi na Serikali kwa ajili ya mafunzo ya anga.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Chuo hicho, Dk Prosper Mgaya wakati wa kongamano la tisa la wahitimu wa chuo hicho ambapo kwa mwaka huu wa masomo watahitimu wanafunzi 2700.
Dk Mgaya amesema NIT wanajitaidi kutoa wanafunzi wenye weledi kwenye njia tano za usafirishaji, ambapo mwaka huu mada yao kuu ipo kwenye usafiri wa reli na wamefanya hivyo kwa sababu za kuzingatia Serikali inavyowekeza fedha nyingi katika usafiri wa reli.
Amesema ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambao umefikia kwa asilimia 95, na kama mnavyoona mabehewa yameshaingia kwamba usafiri utaanza kutumika na pia Serikali imeshasaini mikataba ya ukimaliza kipande kilichobakia.
“Na kama mlivyosikia Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema nchi yetu imekaa kwenye eneo la kimkakati ambayo nchi ya Congo na Burundi zinategemea nchi yetu ndiyo maana reli zitajengwa hadi kwenye hizo nchi ili tuweze kusafirisha mizigo kuja Tanzania,”
“Kwa umuhimu huu, chuo kipo mbioni kuanzisha kitengo cha mafunzo ya usafiri wa reli mkoani Tabora, kita fadhiliwa na Serikali na ndiyo maana chuo kinafanya ukaribu na shirika TRC kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya kuanzisha hicho kituo,”amesema Dk Mgaya
Amesema kuwa ana amini ndani ya mwaka mmoja tayari mafunzo hayo yatakuwa yameanza, lakini sio hivyo tu pia wanategemea kupokea ndege mbili za mafunzo ya upairoti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Uthibiti wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Aridhini (Latra), Johansen Kahatano amesema chuo hicho kinaendelea kutanua wigo wa mitaala kwa kufikia maeneo mengi ya usafirishaji.
Naye mwanzilishi wa kongamano hilo, Injinia Dk Amaon Mwasandube amesema wanachojivunia ni kwamba wameshatoa wahitimu wengi kwenye sekta mbalimbali za usafirishaji na wamefanikiwa kusonga mbele.
“Kikubwa zaidi anaweza kujivunia hata upande wa usalama barabarani tumefundisha vijana wengi kozi za automobile na ukaguzi wa magari sasa hivi vijana wetu wengi ni ma RTO kwa sababu tulikuwa tunawafundisha pamoja na kozi maalum ya ukaguzi wa magari,”amesema
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu