January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIT, ATCL wakubaliana ya kuboresha usafiri wa anga nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Oline, Dar es Salaam.

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeingia katika makubaliano ya ushirikiano mapya na Shirika la Ndege nchini (ATC) katika mipango chanya ambayo italeta manufaa kwenye sekta ndogo ya anga.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kusaini makubaliano mapya katika kampasi kuu ya Chuo hicho Mabibo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi alisema kuwa makubaliano hayo mpya yataleta tija kwa pande zote mbili na kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya anga.

Amesema kuwa wafanyakazi wa sekta ya anga kama marubani, wahandisi na wahudumu wa ndani ya ndege wanatakiwa na sheria kupata mafunzo kila baada ya muda fulani ili kuweza kuhuisha leseni zao na kuwa mara nyingi wamekuwa wakiwapeleka wafanyakazi hao nje ya nchi.

“Ushirikiano huu utapunguza gharama ambazo tumekuwa tukizitumia katika kuwapeleka wahudumu wetu wa ndege wakiwemo marubani kwenye mafunzo nje ya nchi, hivyo makubaliano haya yatawafanya wafanyakazi wetu kupata mafunzo hayo chuoni hapa.

Rubani wetu anaweza kwenda nchini Afrika Kusini kwa mafunzo ya masaa manne hadi matano, na tunatumia gharama kubwa tofauti na ambapo atapata mafunzo haya katika Chuo chetu cha usafirishaji. Tutakuwa tukiwaleta hapa kwa mabasi yetu na hivyo kupunguza gharama.”amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho cha NIT, Mhandisi Prof. Zacharia Mganilwa, amesema kusudio kuu la makubaliano hayo ni kuwezesha taasisi hizi mbili za serikali kushirikiana katika kubuni na kufanya program mbali mbali za mafunzo, kubadilishana ujuzi unaohusiana na sekta ya anga.

Amesema kupitia Shule ya Anga iliyo chini ya NIT wataweza kutoa mafunzo ya usafiri wa anga ya ubobezi ambapo watazalisha wataalamu wengi ambao watasaidia uendeshaji wa Shirika la Ndege la Taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi (Kulia) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Prof. Zacharia Mganilwa wakiongea mara baada ya kusaini makubaliano mapya katika kampasi kuu ya Chuo hicho Mabibo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Mpiga Picha Wetu)

“Tunatarajia kupokea ndege tatu za kufundishia pamoja na vifaa maalum vya mafunzo ya wahudumu wa ndani ya ndege za mafunzo kwa zitakazosaidia wanafunzi nawafanya kazi walio katika sekta ya anga,” amesema.

“Tunatarajia mazungumzo ambayo yanafanyika baina ya wauzaji wa ndege na Benki ya Dunia yatakamilika mapema na hivyo kutuwezesha kupokea ndege hizo za mafunzo kabla ya mwaka huu na kuanza mara moja mafunzo ya urubani,” amesema.

“Chuo kipo tayali kuanza kozi hizo za urubani katika kupunguza uhaba uliopo wa marubani nchini. Tuna waahidi Watanzania kuwa kozi hii ya urubani itaanza kutolewa nchini katika chuo chetu na kuwapunguzia mzigo wazazi kuwapeleka wanafunzi nje ya nchi,” amesema.

Amesema serikali imewekeza zaidi ya Sh. bilioni 50 ambazo zimewekwa kwakipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuzalisha wataalamu wa sekta ya anga.

Prof. Mganilwa amesema alisema kwa kutumia utaalamu mkubwa wa wataalamu waliopo ATCL, wataweza kuwapa mafunzo Watanzania wengine wanaopenda kujifunza juu y ausafiriwa anga, hivyo wanatarajia kupata wataalamu wengi watakaoendesha shirika kwa ufanisi na weledi.

Amesema awali ATCL ilikuwa na ndege mbili, lakini baada ya serikali kuweka uwekezaji mkubwa, sasa shirika lina ndege nane kutokana na serikali ina malengo kuwekeza zaidi katika shirika hilo.

“Tunataka kuliona shirika letu la ndege linakuwa shirika bora zaidi katika ukanda wetu naAfrika kwa ujumla,” amesema.

Aliongeza, “Tunaahidi kuwa tutawekeza zaidi katika kuboresha mafunzo yetu ilituweze kutoa vijana bora watakaoleta tija kwenye sekta ya anga.”

Prof Mganilwa amesema kuwa sekta ndogo ya usafiri wa anga inakuwa kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka .

Zaidi ya hayo, Chuo cha Taifa cha Usafishaji kimejidhatiti kuendelea kutoa mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya kwanza.

Pia Chuo kimeendelea kutoa kozi ya wahudumu wa ndani ya ndege ambapo hadi sasa imekwisha dahili mikupuo miwili kwa mwaka huu wa masomo wa 2020/21.