Na Gibson Bayona
Nahodha imara wa chombo cha majini, umahiri wake haupimwi wakati bahari ikiwa shwari na mawimbi yakiwa yametulia; bali wakati wa dhoruba, mawimbi makali na pepo za kukata na shoka.
Hii ni tafasiri ya Kiongozi imara, hapimwi wakati wa utulivu na mambo yakiwa shwari; Bali wakati wa magumu na nyakati nzito kisiasa, huyu ndie Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt Samia Suluhu Hassan.!
Historia imeandikwa ambapo serikali yetu kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA), imetia saini mikataba mitatu ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na kuhitimisha mjadala wa muda mrefu kuhusu uwekezaji katika lango hili kubwa kwa uchumi wa nchi.
Katika hali isiotarajiwa na wengi, Rais wetu ametoa hotuba yake kwa Taifa kwa umahiri, ufanisi na utulivu mkubwa sana; amezungumza kwa hisia mno akilitanguliza Taifa mbele, akisisitiza juu ya kulindwa kwa Maslahi mapana ya Taifa.
Ni wazi ilikua ni hotuba ya kiumajumui wa Afrika (Pan-Africanist) iliojawa na uchungu, kujitoa na uzalendo wa kweli na utaifa (Nationalism) wa ndani kabisa.
Katika historia ya siasa za Awamu ya 6 ni wazi Kuna mambo kadhaa tunaweza kujifunza katika jambo hili ambalo wengine walidhani lingeligawa Taifa vipande na pengine lingekua changamoto ngumu zaidi katika Uongozi wa Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia amethibitisha umahiri wake katika ustahimilivu wa kusikiliza ukosoaji na hata dhihaka dhidi ya uongozi wake.
Katika mjadala wa bandari yaliibuka makundi mengi yaliyotoa maoni kwa kutumia lugha tofauti, za kistaarabu na zingine za kuudhi, dhihaka na hata matusi lakini Rais wetu alikaa kimya.
Katika kuhitimisha mjadala huu, Rais wetu ameamua kuyaweka mapambano yote yaliojitokeza kama sehemu ya uhuru wetu wa Kujadili na kusema.!
Moja kati ya sifa ya kiongozi mahiri ni utulivu na ustahimilivu wakati wa hatari au shari na uvumilivu wa kukukabali kutokukubaliana na wenye hoja mbadala..!
Hili limejidhihirisha pia kwa Rais wetu kwani kulikua na matukio mengi sana ya kitaifa ambayo Rais angeweza kutumia kujibu au kuzungumzia uwekezaji bandarini lakini alichagua kukaa kimya na kufuatilia maoni ya watu. Maoni kutoka kwa wana CCM, viongozi wastaafu, asasi za kiraia na vyama vya upinzani.
Rais Samia alichagua kuwa na masikio makubwa, lakini mdomo wake ukawa mdogo. Makundi yote yakasema yaliyotaka yazingatiwe kwenye uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam, na mwisho serikali yake ikachambua, ikayachukua yote ya muhimu na leo imetia mikataba ambayo hakika imezingatia maslahi mapana ya Taifa.
Katika jambo lenye kuleta matumaini makubwa na umoja wa kitaifa, Hofu ya DP World kuhodhi bandari zote imeondolewa, serikali imeweka wazi kuwa watawekeza gati namba 4 mpaka 7 tu na gati zingine zitatafutiwa wawekezaji wengine. Hofu kwamba uwekezaji utasababisha ajira za wazawa zipotee serikali imeingia mikataba itakayohakikisha hakuna ajira ya Mtanzania itakayopotea.
Propaganda ya Bandari zote kuhidhiwa imefika mwisho.
Hoja zote muhimu zimezingatiwa na Taifa limebaki na umoja.
Leo hii wanaharakati wameheshimiwa, viongozi wa dini maoni yao yameheshimiwa, Chama kimeheshimiwa,wanazuoni na wajuzi wa mambo wameheshimiwa, na wapinzani wamesikilizwa, Taifa linaongea lugha moja, na haya yote ni matunda ya Uongozi Bora.
Rais Samia anaendelea kuwa mwalimu wa siasa za hoja kwa hoja, uvumilivu, ustahimilivu na kusikilizana.
Sisi viongozi vijana tunaomtazama tunajivunia na kujifunza sana.
Utulivu, Uvumilivu, Ustahimilivu, Ujenzi na uchambuzi wa hoja, Utaifa.
More Stories
Tuhimize amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Ana ahidi,ana tekeleza,maneno kidogo,vitendo vingi
Kwa mafanikio haya, tunastahikumpa kongole Rais Dkt. Samia