October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIC yaja na mkakati kukabili majanga kwenye kilimo nchini

Na Penina Malundo,Timesmajira

SHIRIKA la Taifa la Bima(NIC)imeandaa mkakati mzuri wa kuweza kuyadhibiti na kuyakabili majanga mbalimbali ambayo mkulima anakabiliana nayo ikiwemo Ukame,Mafuriko Magonjwa ya wadudu wasiodhibitiwa au kutibiwa,Vimbunga na Mvua ya mawe.

Miongoni mwa njia itakayokabiliana nayo ni pamoja na Bima ya Kilimo ambayo inalenga kumfidia mkulima pindi anapopata hasara iliyochangiwa na kusababishwa na majanga hayo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ”Sabasaba”,Mtaalam wa Bima ya kilimo na Mifugo,Experius Nchanila
amesema kilimo ni sekta muhimu katika taifa kinachotoa ajira kwa asilimia kubwa ya vijana huku kikichangia pato la taifa,usalama wa chakula kwa ngazi ya familia hadi taifa .

Amesema kutokana na Kilimo kuwa sekta nyeti ni lazima kilindwe,ndio maana NIC imetambua kilimo katika uchumi wa Taifa,Familia na uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa ujumla ambapo imeweza kukaa chini na kubaini changamoto ambazo wakulima wanapitia na kuja na njia ambayo itaweza kuwasaidia.

”Kilimo kimekuwa kikikumbwa na majanga mbalimbali ambayo yanamfanya Mkulima kuathirika moja kwa moja na majanga ambayo yapo nje ya uwezo wa kibinadamu kuweza kuyazuia,”amesema na kuongeza

”Endapo mkulima anakutana na majanga hayo,bima ya NIC inasaidia kurejeshewa thamani,fedha au mtaji kwa mkulima ambae amekuwa amewekeza kupitia kilimo chake ili kumuhakikishia usalama na uhakika wa uwekezaji wake na kumfanya kufikia malengo aliyojiwekea,”amesema Nchanila

Aidha akitaja sifa ambazo mkulima anapaswa kuwa nayo ili kuweza kupata bima hiyo ni pamoja na umiliki wa mashamba,kujua aina ya mbegu au zao analoenda kupanda,kujua historia fupi ya eneo analofanyia kilimo kuanzia kipindi cha miaka mitatu hadi mitano,kuangalia hali ya hewa la eneo husika,Utaratibu wa kilimo bora,tarehe za upandaji wa mazao hayo na kupatiwa dodoso la kutoa taarifa zake za msingi kuhusiana na shamba lake.

Amesema mkulima anapokata bima hiyo anakuwa na uhakika wa kilimo chake na kujikinga na majanga mbalimbali na kumfanya mkulima kuwa kulima kilimo cha tija na faida.