November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni wiki ya joto la uteuzi wa mawaziri

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar

WAKATI Rais John Magufuli akisubiriwa kwa hamu kutangaza baraza lake la mawaziri, joto la nani atakuwemo kwenye baraza hilo linazidi kushika kasi.

Jopo hili linapanda, huku baadhi ya wadadi wa masuala ya kisiasa wakitabiri kwamba Rais Magufuli pengine anaweza kutangaza baraza lake la mawaziri katika wiki inayoanzia leo.

Miongoni mwa wanasiasa wanaozidi kuguswa na joto hilo mi pamoja na wabunge, mawaziri na manaibu wao ambao waliomaliza utumushi wao katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Magufuli.

Rais Magufuli ameishafanya uteuzi wa mawaziri watatu hadi sasa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia alithibitishwa na Bunge kwa asilimia 100 ya kura. Wengine ni Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi.

Ukiondoa mawaziri hao wengine waliokuwa kwenye baraza lake la mawaziri joto lao linazidi kupanda kutokana na kutojua hatima yao. Tayari Rais Magufuli ameshasema wazi kwamba wingi wa wabunge ambao wanatokana na CCM unampa uwanja mpana wa kuchagua mawaziri kwenye Serikali yake.

Kauli hiyo ndiyo inaongeza ugumu wa kujua ni nani kati ya wabunge wa CCM watakaoingia kwenye Serikali yake. Wakati mawaziri na manaibu waziri waliokuwa kwenye Serikali yake wakiwa wanasubiri kwa hamu uteuzi, tayari baadhi ya wabunge wapya wanatajwa tajwa kuwa uenda wakaangukiwa na bahati hiyo.

Kutajwa kwa wabunge hao kuwemo kwenye baraza lake la mawaziri kunatokana na utendaji wao mzuri katika maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine walikuwa wakiyaongoza.

Miongoni mwa wabunge wanaotajwa tajwa kwamba huenda wakawemo kwenye baraza lake la mawaziri ni pamoja na mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei.

Dkt. Kimei anabebwa na sifa ya kuongoza Benki ya CRDB kwa mafanikio makubwa hadi ikawa moja ya benki nchini zinazofanya vizuri na za kutolewa mfano.

Kimei amestaafu hivi karibuni kabla ya kwenda kuwania ubunge Jimbo la Vunjo. Mwingine ni Mbunge wa Kinondoni, Abbasi Tarimba, hasa kutokana na ubobezi wake katika sekta ya michenzo.

Wabunge wengine wanaotajwa tajwa ni mbunge wa Muheza, Hamis Mwijuma, mbunge wa Kawe, Mchungaji Josephat Gwajima na wengine.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kutokana na Serikali ya Rais Magufuli kuahidi mambo mengi kupitia ilani ya CCM na ahadi za papo kwa hapo majukwaani, ni wazi atahitaji mawaziri na manaibu waziri watakaoendana na kasi yake.

“Kasi ya Rais Magufuli katika kipindi cha pili cha uongozi wake itakuwa kubwa sana. Ana mambo mengi ambayo amepanga kuyafanya, hivyo atahitaji watu watakaoendana na kasi hiyo,” alisema mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kiasiasa wakati akizungumza na Majira.

Mchambuzi huyo amesema pengine hiyo, ndiyo imemfanya Rais Magufuli kufanyakazi ya uteuzi kwa umakini mkubwa. “CCM imepata wabunge makini na wenye sifa nyingi.

Ni wazi Rais Magufuli atapenda kuwatumia kwenye uongozi wake ili waweze kumsaidia. Swali hapa anawapataji? Ni lazima awe makini ili kila mmoja apate wizara stahiki,” alisema.