March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni miaka minne ya neema kwa Mashirika ya Umma

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Safari ya miaka minne ya uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ya neema kubwa kwa taasisi za umma na hata kampuni ambazo serikali ina hisa chache.

Ndoto ya Dkt. Samia, tangu ashike hatamu mwezi Machi, 2021, imekuwa ni kuhakikisha nchi inakuwa na mashirika yenye ufanisi mkubwa na wa viwango vya kimataifa.

Kwa hakika, Mkuu huyo wa nchi amekuwa akiishi ndoto yake na ndio maana katika kipindi cha miaka minne, jitihada mbalimbali za kuboresha mashirika ya umma zimeendelea kuchukuliwa.

Katika kipindi hicho cha miaka minne, Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) inayoongozwa na Nehemiah Mchechu, imefanya, na inaendelea kufanya, mageuzi makubwa kwenye taasisi za umma kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji wao.

Serikali imekuwa ikiziwezesha taasisi za umma kimtaji na kutengeneza mazingira ya mashirika ya umma kupata uhuru wa kujiendesha ili kutoa wigo wa ubunifu na hatimaye ufanisi katika utendaji.

Katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya Tanzania imeongeza kwa asilimia 27 uwekezaji katika Taasisi, Mashirika, Wakala za Serikali, na kampuni ambazo ina hisa chache.


Takwimu kutoka OMH zinaonesha kuwa uwekezaji umeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia Sh86.29 trilioni katika mwaka wa fedha 2023/24.

Kiasi hicho cha Sh86.29 trilioni kimewekezwa katika Taasisi, Mashirika, Wakala za Serikali, na kampuni ambazo ina hisa chache 308, kwa ujumla wake.

Ongezeko la uwekezaji huu ni kiashiria cha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuleta mageuzi makubwa katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma.

Ni katika muktadha huo,Dkt. Samia ameyataka Mashirika ya Umma kuendelea kusimamia mageuzi yanayofanywa na Serikali kwa lengo la kuongeza tija kwa wananchi na kuwezesha Mashirika hayo kujitegemea.

Rais Dkt. Samia alitoa wito huo hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kiliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

“Safari ya mageuzi kwenye Mashirika ya Umma inaendelea— tayari matokeo chanya yameanza kuonekana ikiwemo kuongezeka kwa mapato, hali ya kujiamini ndani ya Mashirika na katika ubunifu wa watendaji,” Rais Samia alinukuliwa akisema.

Kutokana na mazingira mazuri yaliyotengenezwa na Serikali ya awamu ya sita, Mashirika ya Umma kwa sasa yako kwenye nafasi ya kupanua uzalishaji na utoaji wa huduma.

Mfano mzuri ni Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) ambalo limeweza kuongeza umiliki wake wa Kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay kutoka asilimia 20 hadi 40.

Hii haiishii kwa mashirika ya umma tuu, inaenda mbali kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache na mfano mzuri ukiwa ni Kiwanda cha Saruji Mbeya, ambacho Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inamiliki asilimia 25 ya hisa zake.

Serikali, kupitia OMH, na kampuni ya AMSONS, Oktoba mwaka jana, waliingia makubaliano ya kuwekeza $320 milioni (yapata Sh784bilioni) katika upanuzi wa kiwanda hicho na kuanzisha kiwanda kipya cha saruji Tanga, asante kwa mazingira wezeshi ya biashara.

Kati ya fedha hizo, $190 milioni (yapata Sh465.5 bilioni) zitatumika kwaajili wa ujenzi wa kiwanda kipya Tanga na $130 milioni (Sh318.5 bilioni) ni kwaajili ya upanuzi wa kiwanda cha Saruji Mbeya.

Sanjari na hilo, ikiwa ni matokeo ya mageuzi kwenye mashirika ya umma, Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, mwaka 2023 ilipata gawio la Sh3 bilioni kutoka kwa Kiwanda cha Saruji cha Mbeya, ikiwa ni miaka 10 ipite bila kampuni hiyo kutoa gawio.

Aidha, akizitaka taasisi za ummaa kukumbatia ubunifu,Rais Samia alitoa heko kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira-Tanga (Tanga-UWASA) kutumia Hati Fungani (Bond) kupata jumla ya Sh54.72 bilioni kama njia mbadala ya kupata mtaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji na utunzaji wa mazingira.

Juhudi hizi za mashirika ya umma ni mwitiko kwa Serikali juu ya haja ya mashirika ya umma kupunguza utegemezi serikalini.

“Ninatoa pongezi kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo kufuatia mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali, limeanza kupata faida na kuanza kulipa mishahara ya watumishi wake,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Mchechu, muda wote amekuwa akisema kuwa ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania.

“Sisi kama Serikali tumejidhatiti kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kutunga sera rafiki zinazohamasisha uwekezaji nchini kwa nia ya kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii,”anasema Mchechu.

Hali kadhalika,Mchechu anawataka viongozi wa Mashirika ya Umma kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.

“Uwekezaji wa Sh86.3 trilioni ni mkubwa sana. Tunahitaji kuona matokeo chanya ya uwekezaji huu,”amesema Mchechu.

Pia, anasisitiza umuhimu wa Mashirika ya Umma kufanya utafiti wa kutosha kuhusu uwekezaji ili kukwepa kutumia fedha za walipa kodi bila matokeo.

Dkt. Daudi Ndaki, Mtaalamu wa Uchumi na Uwekezaji kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe anampongeza Rais Samia kutokana na msisitizo wake mkubwa juu ya haja ya uboreshwaji wa Mashirika ya Umma.

Tangu aingie madarakani, Rais Samia amekuwa kinara katika kutoa msisitizo juu ya umuhimu wa viongozi kukumbatia uwajibikaji, ubunifu, na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

“Mhe. Rais Samia amebadilisha mtizamo wa mashirika ya umma kutoka kuitegemea Serikali kuu kwenda kwenye kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli zao,” amesema Dkt Ndaki hivi karibuni.

Ameongeza: “Hii inadhihirishwa na wakuu wa taasisi mbalimbali ambao kwa sasa wanafikiria masula ya hati fungani kama chanzo cha kupata pesa za kuendeshea taasisi zao.”

Dkt. Lutengano Mwinuka, Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ameelezea miaka minne ya Rais Samia kama chachu ya kuimarisha utawala na utendaji wa taasisi za umma ili ziweze kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.

Wimbo wa Rais umekuwa ni haja ya Bodi na Wakuu wa Taasisi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha kwamba taasisi wanazo ziongoza zinatoa huduma bora na zenye tija kwa wananchi.

“Kumekuwa na uelekeo wa mageuzi. Mhe. Rais anataka mageuzi kwenye mashirika ya umma na lengo likiwa ni kuongeza mchango wao kwenye mfuko mkuu wa Taifa,” alisema Dkt Mwinuka.

Kwa sasa, mchango wa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kutoka kwa Mashirika ya Umma na kampuni ambazo serikali ina hisa chache uko katika asilimia tatu tuu ya mapato ya ndani ya nchi.
Ni katika muktadha huo, Mhe. Rais Dk. Samia Agosti mwaka jana alitoa maigizo kwa mashirika hayo kuongeza mchango wao hadi kufikia asilimia 10 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mtizamo wa Serikali ya awamu ya Sita ni kuwa na mashirika ya umma yatakayokuwa na tija kwa Taifa, kwa gharama yoyote, hata kama ni kwa kuyaunganisha au kufuta mengine.

Hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya uchambuzi ambao ulibainisha kuwepo kwa taasisi ambazo zinatekeleza majukumu yaliyopitwa na wakati au yanayo tekelezwa na taasisi nyingine za umma (duplication in roles).

Hivyo mapendekezo yalitolewa, na Serikali kuridhia kuunganisha na kufuta baadhi ya taasisi ambapo Disemba 15,2023 Serikali ilitangaza uamuzi wa kuunganisha taasisi 16 kwa kuunda taasisi saba na kufuta taasisi nne.

Maamuzi hayo ya Serikali yanalenga kuboresha na kuleta tija katika mikakati na malengo mbalimbali yanayo tekelezwa katika mashirika na Taasisi za umma.