Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mjumbe wa Kamati Kuu Ccm Taifa, Laila Ngozi amesema wanawake wa Tanzania wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi za uongozi kwa kundi hilo, kwani ingekuwa vigumu wanawake kuingia kwenye asilimia 50 kwa 50 ya uongozi.
Mjumbe wa Kamati Kuu Ccm Taifa, Ngozi ameyasema hayo juzi wakati wa kongamano la mabinti na wanawake Mkoa wa Tanga katika kuazimisha siku ya wakina mama Duniani iliyoandaliwa na Taasisi ya Wanawake na Uongozi chini ya Mkurugenzi wake Shamira Mshangama.
Amesema miongoni mwa changamoto ambazo zilikuwa zikiwarudisha nyuma watoto wa kike katika suala zima la kugombea na kupata nafasi za uongozi ilikuwa ni suala la rushwa ya ngono.
“Rais wetu siyo mbinafsi anawapenda wanawake na wanaume anaongoza jinsia na makundi yote, amewawezesha na akaona atakapomaliza muda wake wa uongozi atapata mwanamke mengine na kuacha alama kubwa sana” amesema.
Sambamba na hilo Ngozi amemuelezea Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake na Uongozi kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na wasifu pamoja na mambo mengi aliyofanya kwa mabinti na wanawake mkoani Tanga.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya Wanawake na Uongozi, Mshangama amesema lengo kubwa la taasisi hiyo ni kuwezesha wanawake pamoja na mabinti wenye changamoto mbalimbali hususani katika nafasi ya uongozi ili kufikia malengo yao.
Aidha ameushukuru uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuweka ukomo wa nafasi ya uongozi wa Ubunge viti maalumu kwani ni moja ya changamoto zilizokuwa zikiwakumba mabinti ambao wana uwezo lakini hawapati nafasi ya kugombea.
“Wapo wanawake wengi katika nafasi za Ubunge viti maalumu, Ilikuwa ni changamoto kubwa ambayo iliwanyima fursa vijana wengi waliotaka kugombea nafasi za uongozi, tunaipongeza Ccm kwa kuweka ukomo wa kugombea nafasi hizo.

“Sisi Wanawake na Uongozi tumefanya tafiti na tukagundua ni vigumu kwa mabinti kushika nafasi za uongozi hasa Ubunge wa viti maalumu, mabinti wengi wamefutiwa ndoto zao za kuwa viongozi kwa sababu ya rushwa ya ngono” amesema.
Awali akizungumzia maendeleo ya miaka minne ya Rais, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaunganisha wanawake kwa ushupavu wake na kuondoka zana iliyokuwa imejengeka ya wanawake kubaguana katika nafasi mbalimbali hasa za uongozi.
Dkt. Buriani pia amebainisha kwamba miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita kila sekta imeguswa katika maendeleo na hadi kufikia ilani ya uchaguzi itakuwa imekamilika kwa asilimia zote.

Amesema uwekezaji mkubwa wa bandari ya Tanga umezaa matunda makubwa ambapo mapato yanazidi kuongezeka huku vijana wengi walipata ajira, sambamba na hilo ujenzi wa kiwanja cha ndege mkoani humo tayari mchakato wa manunuzi umeshaanza.
“Shilingi Trilioni 3.2 tumeletewa katika Mkoa wetu wa Tanga kutekelezea miradi ya maendeleo ikiwemo kwenye sekta mbalimbali kama vile afya, elimu na miundombinu, Muheshimiwa Rais amefanya makubwa katika uongozi wake” amesema.
More Stories
Wataalamu wa ujenzi mfumo wa NeST wanolewa usalama wa mifumo
Mkurugenzi Rapha Group aeleza fursa mashindano Tulia Marathoni
Prof.Muhongo amshukuru Rais Samia kwa fedha nyingi miradi ya elimu Musoma Vijijini