Na Joyce Kasiki, Tomesmajira Online – Dodoma
MKURUGENZI wa Huduma za Msaada wa Kisheria ambaye pia ni Maajiki wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria , Ester Msambazi, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kutoa huduma ya msaada wa kisheria, ili kufikia wananchi wengi zaidi na kuwapa uelewa wa kina juu ya masuala ya kisheria.
Msambazi ameyasema hayo leo, Agosti 12, 2025, jijini Dodoma katika Kongamano la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali 2025 lililoanza Agosti 11 na linalotarajiwa kufikia tamati yake kesho, Agosti 13, 2025.
“Tumejifunza kuwa tukishirikiana kwa pamoja, tunaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi. Kwa mfano, kupitia kampeni mbalimbali, tumewafikia wananchi zaidi ya milioni nne. Wizara imeanzisha madawati ya msaada wa kisheria tangu Novemba mwaka jana, na tayari zaidi ya wananchi milioni 10 wamepata huduma hiyo,” amesema Msambazi.
Ameongeza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria nayo yamefikia wananchi zaidi ya milioni tano. “Hii ina maana kuwa kwa ujumla, wananchi karibu milioni 20 wamefikiwa na huduma hii ya msaada wa kisheria,” amesema.
Amesema bado wananchi wengi wanahitaji elimu kuhusu masuala ya kisheria, huku akiweka bayana kuwa migogoro mingi inayowakabili imekuwa ikichukua muda mrefu kutatuliwa. Migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa hutatuliwa na serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Katika hatua nyingine, Msambazi amesema kuwa wakati wa utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria iliyopewa jina la Mama Samia Legal Aid Campaign, baadhi ya migogoro ya wananchi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 18 hadi 20 ilitatuliwa.
Aidha, amesema kampeni hiyo ambayo ilipangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, imefanikiwa kufikia lengo lake kabla ya muda kwa kufika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Visiwani. “Katika kampeni hiyo, tumekutana na migogoro zaidi ya 26,000, ambapo migogoro 6,000 ilitatuliwa papo hapo,” amesema.
Kwa mujibu wa Msambazi, kupitia kampeni hiyo waliweza pia kuwaandalia wananchi 1,346 nyaraka muhimu, akibainisha kuwa kampeni hiyo imetekelezwa hadi ngazi ya vijiji ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma kwa karibu.
Amesisitiza kuwa kampeni hiyo imelenga kupanua wigo wa upatikanaji wa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria, uwakilishi mahakamani kwa wananchi wenye mashauri, pamoja na uandaaji wa nyaraka kwa ajili ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Vile vile, amesema kupitia kampeni hiyo imebainika kuwa huduma ya msaada wa kisheria inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa amani, usawa na maendeleo ya wananchi mmoja mmoja.
“Hii ni kwa sababu inapunguza muda wa wananchi kutafuta haki, na badala yake muda huo unatumika kufanya shughuli za kiuchumi, hivyo kuchangia katika pato la taifa,” amesema Msambazi.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako