November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NGAIZA FOUNDATION wasimama na Rais Samia kupigania elimu bora kwa mtoto wa kike

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Shirika lisilo la Kiserikali la NGAIZA FOUNDATION limesema litaendelea kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan katika jitiada anazofanya kuboresha suala la Elimu hususani kwa mtoto wa kike ambapo limesema uamuzi wake wa kuruhusu Wanafunzi wa kike waliokuwa wamepata ujauzito kurejea shuleni ulikuwa na tija kubwa Sana katika kumkwamua mwanamke.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Eizabeth Ngaiza amesema katika kuelekea siku ya Wanawake Duniani March 08, Wanawake tunajivunia kupata Rais Shupavu mwanamke ambae licha ya kuliongoza vizuri Taifa pia ameonyesha dhamira ya dhati kumkwamua Mtoto wa kike hususani pale alipotangaza kuruhusu Wanafunzi wa kike waliopata ujauzito kurejea shuleni.

Kutokana na hilo Ngaiza ametoa wito kwa Wananchi na Wanawake nchini kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili aweze kutimiza maono makubwa na mapana aliyoyabeba kwa maslahi ya Taifa.

Aidha Ngaiza amesema kwakuwa sheria ipo na inafanya kazi ni vyema wanaohusika kuwapa ujauzito Wanafunzi wakaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ili iwe fundisho huku akiwataka Wazazi kuacha tabia ya kumaliza masuala hayo kifamilia.

Hata hivyo Ngaiza amesema katika Kampeni ya NIACHE NISOME inayolenga kupambania usawa wa Elimu kwa mtoto wa kike inayoendeshwa na shirika hilo wamekutana na Kilio Cha Wazazi wanaolalamikia kutozwa fedha za ununuzi wa Madawati licha ya Serikali kununua Madawati ambapo wameiomba Serikali kulitazama suala hilo.

Itakumbukwa kuwa Rais Samia alisema suala la kurudi shule haliwahusu wanafunzi waliopata mimba pekee bali wanafunzi wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, ujauzito na nidhamu ili kutoa fursa kwa watoto wa Tanzania kupata elimu.