Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU chache kuelekea maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka watanzania kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji na kufanya shughuli endelevu za kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa watanzania watumie siku hiyo kama sehemu ya kutafakari umuhimu wa mazingira kwa faida ya kizazi cha leo na kesho.
“Tunasherehekea siku ya mazingira duniani kila mwaka ifikapo June 5, ni siku muhimu kwa watanzania na dunia kwa ujumla kutafakari na kuchukua hatua katika utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na ufanyaji wa shughuli endelevu za uchumi,’’ amesema Dkt. Gwamaka.
Dkt. Gwamaka pia alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kushiriki katika utunzaji wa mazingira ili kuvinusuru viumbe vingine vilivyopo katika mazingira.
“Mazingira yanahusisha viumbe hai na visivyo hai, hivyo tunafanya shughuli zetu za maendeleo ni lazima kuangalia utegemezi uliopo, nawaomba wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji kufanya shughuli zao huku wakishiriki utunzaji wa mazingira,’’ amesisitiza.
Aidha amesema kuwa, kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Lindi ambapo Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan atalihutubia taifa kupitia runinga na vituo mbalimbali vya radio.
“Maadhimisho haya yatafanyika kitaifa mkoani Lindi sambamba na kuzingatia maelezo ya Wizara ya Afya ya kuzuia mikusanyiko ili kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona,’’ amesema Dkt. Gwamaka.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa NEMC, Fredrick Mulinda amesema kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa miongoni mwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na kuitaka jamii kuchukua hatua Madhubuti kukabiliana na hali hiyo.
“Mabadiliko ya tabia nchi yanaleta madhara makubwa katika mazingira ikiwemo kupotea kwa baadhi ya mimea na viumbe vingine hivyo jamii lazima ijikite katika kufanya shughuli zake kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam wa mazingira,’’ amesema Bw. Mulinda.
Ameongeza kuwa kadiri joto linavyoongezeka kumekuwa na upotevu wa viumbe hai na mimea ambayo ni muhimu kwa chakula na kutengeneza madawa.
“Tunapoazimisha siku ya mazingira duniani yatatupasa kukumbuka umuhimu wa kuyatunza mazingira yetu ambayo yamekuwa muhimu kwa ustawi wa mimea na viumbe hai, hali ya kutegemeana ni kitu ambacho kunapaswa kuangaliwa na kila mdau wa mazingira,’’ amesema.
Siku ya Mazingira duniani mwaka huu kimataifa itaazimishwa nchini Colombia ambapo mada kuu itakuwa bionuwai (Biodiversity).
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme