November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NEMC yasitisha shughuli za mwekezaji kijiji cha Buyuni

Na Penina Malundo.timesmajira,online


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeweka zuio la kusitisha shughuli za mwekezaji wa uchimbaji chumvi anayefanya shughuli hizo katika kijiji cha Buyuni wilayani Pangani mkoni Tanga jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
NEMC imefikia hatua hiyo baada ya mwekezaji huyo, kutokana na uwekezaji wake kutishia maisha ya wanyamapori waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani pamoja na kuwepo kwa uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

Zuio hilo limetolewa mwishoni mwa wiki,wilayani Pangani na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Samuel Gwamaka wakati wa ziara ya kukagua eneo hilo, alisema NEMC imeweka zuio hilo kutokana na mwekezaji wa eneo hilo kutofata taratibu za kimazingira pindi anapoanza kutekeleza mradi huo wa uvunwaji wa chumvi katika eneo hilo.

Amesema wamesimamisha shughuli hizo baada ya kugundua kuwa kimazingira eneo hilo ni nyeti hususani kwa wanyama mbalimbali  wakiwemo Tembo wanaotokea hifadhini na kutembea wakati mwingine kukaa kabisa.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Samuel Gwamaka akizungumza na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephrahim Mwangomo katika kijiji cha Buyuni wilayani Pangani katika mradi wa uvunwaji wa chumvi ambao umekua ukiathiri mazingira katika eneo hilo.

Gwamaka amesema endapo mwekezaji huyo atakiuka amri hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwani baraza  limemtaka mwekezaji wa mradi huo kuwathibitishia kama alifanya tathimini  ya athari ya mazingira kabla ya kuanza kwa mradi huo na kujua ni athari gani zingeweza kujitokeza pindi wanafanya shughuli za uchimbaji wa matuta( vyungu) vya kuvunia chumvi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephrahim Mwangomo amesema eneo ambalo mwekezaji huyo anafanyia shughuli zake ni moja kati ya maeneo muhimu ya mbuga ambayo utumiwa na tembo kujipatia chakula.
Amesema mwekezaji huyo alipokwenda ofisini kwao walimshauli kubadirisha matumizi eneo hilo kwa kuacha kuchimba chumvi na kufikiria kujenga hoteli kwa ajili ya watalii.
 
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Buyuni kilichopo kata ya Mkwaja Wilaya ya Pangani, Diwani Waziri amesema, kuwa mradi huo wa uchimbaji chumvi unaomilikiwa na mwekezaji ulioanza mwaka 2015 na alipewa na kijiji heka 50 ili aziendeleze na kufanya maendeleo katika kijiji hicho.
Amesema mwekezaji huyo amekuwa akiwasaidia katika huduma mbalimbali za jamii ikiwemo kuwachimbia mabwawa ya kupokea maji ya mvua.
“Pamoja na kwamba mwekezaji huyu tulimpatia heka 50 ili azitumie kwa shughuli zake, tunakiri kwamba hatukuwashirikisha TANAPA wakati wa kufanya maamuzi ya haya mambo,” amesema.