Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC)limesema linaendelea na Utafiti Kuhusu Uwezo wa Kuoza kwa Mifuko Mbadala ya Non-Woven.
Ambapo Utafiti huo unafanyika kuainisha ubora na viwango vinavyotakiwa kuzingatiwa katika utengenezaji wa mifuko mbadala isiyo ya plastiki ili kujua uwezekano wa mifuko hiyo kuwa na uwezo wa kuoza.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 24,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt.Immaculate Semesi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha Dkt.Semesi amesem zaidi ya tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria.
“Suala la udhibiti wa vifungashio vya plastiki ni letu sote, hatuna budi kushirikiana kwa ajili ya kuleta matokeo chanya,”amesema Dkt.Semesi.
Vilevile amesema Baraza hilo limefanya tafiti mbalimbali na kuaandaa maandiko ya miradi ambapo limeratibu utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi, kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu pamoja na mradi wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya mazingira.
“Ajenda ya tafiti imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja utafiti kuhusiana na changamoto za uchafuzi wa Mto Mara,Mmomonyoko wa fukwe za maeneo ya Coco Beach,Kunduchi Beach,Mbweni JKT Beach Club na KJ742 Navy,Fukwe za Mikadi, eneo la Msuka lililopo Pemba Kaskazini, Ghuba ya Mikindani na Manispaa ya Mtwara,”amesema.
Pamoja na hayo Dkt.Semesi amesema Baraza limefanya tathmini ya hali ya mazingira kwenye maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi katika milima ya Hanang, Manyara na Mamba Myamba iliyopo Wilayani Same – Kilimanjaro.
Hata hivyo Dkt.Semesi amesema NEMC imefanya jumla ya kaguzi 9,606 na malalamiko 1,483 yalishughulikiwa hasa katika eneo la kelele na mitetemo.
Ambapo Uchafuzi wa mazingira ulidhibitiwa katika miradi mikubwa yenye viashiria hatarishi ambapo programu 50 za elimu na vipindi 75 vya uhamasishaji vilifanyika.
Pia amesema jumla ya vibali 781 vilitolewa kwa wafanyabiashara mbalimbali na nyaraka 1,477 za ufuatiliaji zilitolewa ambapo 1,089 zilirejeshwa na kufanyiwa mapitio na kubaini kuwa tani 165,834 za taka hatarishi zilifuatiliwa kwa mafanikio kote nchini.


More Stories
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.Â
Samamba:Uongezaji thamani madini ni mkakati wa serikali kukuza mchango wa sekta
Prof.Muhongo apongezwa kuleta majadiliano sekta ya elimu Musoma