October 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NEMC yaeleza jitihada za serikali zilivyotokomeza ugonjwa wa kipindupindu kwa miaka saba mfulululizo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

BARAZA la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC)limesema jitihada  za serikali za kusisitiza usafi wa mazingira zimeleta mafanikio makubwa ikiwemo kutomeza ugonjwa wa kipindupindu ambao haujaripotiwa tena kwa miaka saba sasa.

Hayo yamesemwa jijini leo,Machi 3,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Samweli Gwamaka wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa baraza hilo  katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha usafi wa mazingira  ikiwa ni pamoja na kuhamasisha usafi wa kila jumamosi na  elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo jitihada hizo zimesaidia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu.

 “Miaka  ya nyuma  ikifika kipindi cha mvua lazima wapatikane wagonjwa wa kipindupindu lakini sasa hivi kutokana na elimu inayotolewa  jamii imegundua kuwa ikiwa katika mazingira machafu na magonjwa yanaweza kuiandama,”amesema Dkt.Gwamaka.

Hata hivyo Dkt.Gwamaka ameeleza kuwa  NEMC imepanga kuanzisha klabu za utunzaji wa mazingira kuanzia  ngazi ya shule za msingi na sekondari ili kuwajengea watoto  msingi mzuri wa namna ya kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.

Ameeleza NEMC inaanzisha klabu za mazingira na kuzilea  kwasababu watoto  wakianza kufundishwa wakiwa katika umri mdogo ni rahisi zaidi kuelewa umuhimu wakutunza mazingira na faida zake kijamii,kiuchumi na kiafya.

“Tunaenda  kuelimisha na kukikamata kizazi cha watoto wadogo kuanzisha shule za msingi na sekondari ili wachukulie suala la utunzaji wa mazingira ni jukumu lao la kila siku katika mwenendo mzima wa maisha yao.Tunaamini watakapo kuwa wakubwa tabia itakuwa imejengeka ,”alisema .

Dk.Gwamaka alieleza kuwa NEMC imeendelea kupokea na kushughulikia malalamiko taklibani 369 ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi ikiwemo kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye bomba,kuchoma taka hatarishi chini ya kiwango,uchafuzi wa vyanzo vya maji,utiririshaji wa maji taka na uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwanda.