December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC), Dkt.Samuel Gwamaka, akizungumza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dar es salaam ambapo(NEMC) juu ya kero wanazopata wananchi wanaishi karibu na kumbi za starehe,mabaa pamoja na baadhi ya nyumba za ibada nyakati za usiku ambapo ni uvunjifu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni yake inayosimamia kelele na mitetemo ya mwaka 2015 inayotaka kudhibiti kelele. Na mpiga picha wetu.

NEMC kuwaburuza mahakamani wachafuzi kelele na mitetemo

Na Mwandishi Wetu

KUFUATIA kuwepo kwa wimbi kubwa la uchafuzi wa kelele na mitetemo jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesemaonyea kwamba litawafikisha mahakamani wahusika wote kama hatua ya kudhibiti hali hiyo.

Akizungmza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka, alisema baraza halitomuonea mtu bali hatua zitachukuliwa kukidhi matakwa ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni ya uchafuzi wa kelele na mitetemo ya mwaka 2015.

“Sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni yake inayosimimia uchafuzi wa kelele na mitetemo ya mwaka 2015 imeweka wazi viwango vya sauti katika viwanda, maeneo ya biashara pamoja na maeneo ya taasisi za elimu. NEMC tutaitumia sheria hiyo kuhakikisha changamoto hiyo inaondoka na kuwapa utulivu wa kutosha wananchi,” alisema Dkt. Gwamaka.

Alisema kuwa NEMC imechukua hatua kadhaa kuhakikisha wenye mabaa, kumbi na nyumba za starehe wanadhibiti uchafuzi wa kelele na mitetemo lakini wimbi la uchafuzi huo limeongezeka na ushahidi ni kuongezeka kwa malalamiko ya wananchi.

“Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na kelele zinazotoka katika kumbi za starehe, mabaa na baadhi ya nyumba za ibada.

NEMC tumechukua hatua kadhaa ikiwemo kutoa elimu, kuwaonya baadhi ya wahusika na utozaji faini lakini malalamiko yameongezeka na tumejipanga kuchukua hatua za juu zaidi na kuwafikisha mahakamani,’’ amesema.

Dkt. Gwamaka amesema kelele hizo zimekuwa kero kwa wakazi wa maeneo husika hususani kushindwa kusoma kwa utulivu, kuwaathiri wagonjwa pamoja na wananchi kushindwa kupata mapumziko mazuri, hasa nyakati za usiku.

“Wananchi wanakosa muda mzuri wa kupumzika hasa nyakati za usiku na kwa kufanya hivyo inawafanya washindwe kuwa na ufanisi katika shughuli zao za uzalishaji mali. Baraza limejipanga kuhakikisha changamoto hiyo inafika mwisho kwani sheria imeeleza wazi hatua za kuchukua kwa wanaokiuka sheria,’’ amesema.

Aidha amewashauri wamiliki wote wa kumbi na nyumba za starehe, baa na nyumba za ibada kujenga majengo ambayo yatakuwa yanazuia sauti isisafiri umbali mrefu na kusababisha madhara kwa wananchi wengine.

“Sio kusudio la NEMC kuwafanya watu wasifanye biashara au kuzuia uhuru wa mtu kustarehe au kufanya ibada bali wafanye hivyo kwa kufuata sheria na kanuni ambazo haziwezi kuwanyima wengine fursa ya kupata mapumziko na utulivu.

Baraza linawashauri wenye mabaa, nyumba za starehe pamoja na nyumba na ibada kuwa na majengo ambayo yatazuia masafa ya sauti yasisafiri umbali mrefu na kuathiri watu wengine,’’.