Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Kasulu
WAKULIMA zaidi ya 2000 Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma,wameanza kunufaika na zao la mchikichi baada ya kupatiwa mbegu ya kisasa aina ya tenera ambayo inastahimili ukame na kuzaa matunda mengi.
Wakiongea na mwandishi wa Timesmajira Online,aliyekuwa wilayani humo hivi karibuni baadhi ya wakulima wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa serikali wa kugawa bure mbegu bora za zao hilo ambazo hustawi vizuri na kutoa matunda mengi.

Sadoki Mgama, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Kiyungwe, Kata ya Kitanga wilayani humo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia miche zaidi ya laki 3 katika kata hiyo.
‘Mbegu hii inaanza kuzaa matunda baada ya miaka 3 tu, baada ya hapo tunaanza kuvuna mfululizo, sasa hivi nimelima hekali 44 na kwa awamu hii ya kwanza natarajia kuvuna lita laki 1 za mafuta ya mawese, hivyo kunufaika zaidi,”amesema Mama na kuongeza:
‘Licha ya kwamba tunalima na mazao mengine, zao hili ni fursa muhimu sana kwetu kwa sababu linatoa matunda mengi, haliathiriwi na wadudu wala ukame na litatuwezesha kuendelea kuvuna hadi uzeeni,”.
Kaimu Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Masumbuko Kwelemwa,amesema kuwa hadi sasa wakulima wapatao 2,443 wamepatiwa miche ya zao hilo na kuipanda, awali walikuwa na hekali 20 tu lakini sasa hekta 1,406 zimepandwa.
Amebainisha kuwa kutokana na Wilaya hiyo kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha zao hilo na mazao mengine, wananchi wengi wamehamasika kuchukua mbegu hizo na hadi sasa jumla ya miche 175,650 imeshagawiwa kwa wakulima.
Ametaja Kata ambazo zimeanza kunufaika na kilimo hicho kuwa ni Rusesa, Bugaga na nyinginezo na elimu zaidi inaendelea kutolewa ili wakazi wa kata zote katika halmashauri hiyo waanze kulima zao hilo ili kuneemeka kiuchumi.

Kwelemwa ameeleza kuwa,matarajio ya halmashauri hiyo ni kuongeza uzalishaji ili waweze kufikisha mavuno ya tani 300,000 za zao hilo na kupata mafuta ya kutosha ya mawese ili kunufaika na soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa zao hilo ni miongoni mwa mazao manne ya kibiashara yaliyopewa kipaumbele kikubwa katika halmashauri hiyo ili kuzalishwa kwa tija na kuwezesha wananchi kunufaika zaidi, mazao hayo ni kahawa, alizeti na pamba.
.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi