Na Judith Ferdinand, Mwanza
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa mafunzo kwa waratibu wa mikoa, wasimamizi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi, maofisa ugavi na maofisa uchaguzi kutoka Mikoa ya Mwanza na Mara ikiwataka watimize vyema wajibu wao kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wadau hao jijini Mwanza leo Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, amesema tume imewaamini na kuwateu kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Amesema wanapaswa wajiamini,kujitambua na kuzingatia Katiba ya nchi, Sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili na maelekezo yanayotolewa na NEC katika kutekeleza majukumu yao.
“Tumewakutanisha ili mbadilishane uzoefu,kujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,”amesema.
Pia amewahimiza kujifunza kwa vitendo mambo muhimu katika mchakato wa uchaguzi ikiwemo ujazaji sahihi wa fomu mbalimbali,ufungaji wa vituturi, kufunga na kufungua masanduku, mpangilio wa kituo na taratibu za upigaji kura sanjari na kuyajua vyema maeneo yao ya kufanyia kazi ikiwemo hali ya kisiasa na miundombinu ya kufika katika kata na vituo husika.
” Katika utekelezaji wa majukumu yenu ni muhimu pia mvishirikishe vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kwa uwazi katika masuala ambayo wanastahili kushirikishwa ili kujenga umoja kuanzia hatua ya awali hadi siku ya kutangazwa matokeo hii itasaidia kuondoa migogoro,vurugu,uvunjifu wa amani,kuharibika kwa uchaguzi na kusababisha hasara kwa Derikali na maisha ya watu,”amesema.
Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuhakiki na kubaini mahitaji sahihi ya kila kituo na kutatua changamoto mapema kabla ya siku ya kupiga kura.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, amesema wamejiandaa vyema kupokea mafunzo hayo ,hivyo hawatawaangusha bali wataitendea haki elimu hiyo watakayoipata.
Naye Mkurugenzi wa Jimbo la Musoma Mjini, Fidelica Myovella akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo anasema watatumia muda huo wa siku tatu kusikiliza kwa umakini,uaminifu na utii ili kuhakikisha yote wanayofundishwa wanayazingatia lengo likiwa ni kuwafikishia elimu hiyo kikamilifu wenzao katika maeneo ya uchaguzi watakayoenda.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi