December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa NEC, Wilson Mahera

NEC yatangaza rasmi waliopita bila kupingwa

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewatangaza wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo 18 waliopita bila kupingwa.

Akitangaza majina hayo jana Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa NEC, Wilson Mahera amesema wagombea walipita bila kupingwa ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi wa NEC, Wilson Mahera

Amewataja wagombea hao kuwa ni Elias Kwandikwa (Ushetu), Job Ndugai (kongwa), Ahmed Shabib(Gairo), Prof Paramagamba Kabudi (Kilosa), Jonas Zeeland (Mvomero) na Kalogereris Innocent (Morogoro Kusini).

Wengine  ni Taletale Shabani (Morogoro Mashariki), Mhandisi Isack Kamwelwe (Katavi), Godfrey Pinda (Kavuu), Pilipho Mulugo(Songwe), Selemani Zedi (Bukene) na Dkt Hamis Kigwangala (Nzega Vijijini).

Wagombea wengine waliopita bila kupingwa ni Kassim Majaliwa (Ruangwa), Nape Nauye (Mtama), Vita Kawawa (Namtumbo), Jumanne Sagini (Butiama), Alexzanda Mnyeti (Misungwi) na January Makamba (Bumbuli)

Dkt Wilson amesema tume itaendelea kutoa taarifa za wagombea wanaopita bila kupingwa kwa kadri watakavyo kuwa wanapata taarifa kwa wasimamizi wa majimbo.

Pia Dkt.Mahera ametumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wagombea na vyama vya siasa kuingilia mchakato wa kisheria unaosimamiwa na NEC katika maswala ya mapingamizi.

“Mfano mgombea Urais wa CUF na CCM waliwekewa pingamizi na mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, lakini hii pia ni kwa mujibu wa sheria kwamba wanaopaswa kuweka pingamizi kwenye ngazi za urais ni pamoja na mgombea anaweza akaweka pingamizi,

“Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza akaweka pingamizi, Mkurugenzi wa Uchaguzi anaweza akaweka pingamizi kwa hiyo tumeweka utaratibu na sheria inataka hivyo kwa hiyo wanapoweka pingamizi wanasema tume inatakiwa baada ya muda mfupi umjulishe aliyewekewa pingamizi kwa maandishi ili na yeye ajibu alafu tume ifanye uamuzi,” amesema Dkt Mahera.

Amesema tume ilifuata utaratibu wala haikutishwa lakini ilifanya kazi yake vizuri mapingamizi yalipokelewa na Tume ikakaa,ikachambua kwa mujibu wa sheria na taratibu na ikatoa matokeo ya uchambuzi wa hayo mapingamizi bila kutishwa na kazi ilienda vizuri.

Hata hivyo amesema kumezuka tabia ya baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wachache kuingilia mchakato wa kisheria unaosimamiwa na NEC mfano maswala ya uchaguzi.

Amewataka viongozi wa vyama vya siasa waache kuwatisha watendaji wa Tume wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria,taratibu na kanuni.

Aidha alisema,wagombea ambao hawataridhika na maamuzi ya pingamizi zinazowekwa wanayo fursa ya kukata tufaa kwa Tume na muda wa kukata rufaa umewekwa kwa mujibu wa kifungu cha 40(3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 303.