November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndungulile afungua mkutano wa 41 wa SATA wa nchi za SADC

Na Faraja Mpina,TimesMajira online, Dodoma

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amefungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Sourthern Africa Telecom Association (SATA) ambapo nchi ya Tanzania kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imekuwa mwenyekiti wa Umoja huo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kulia) akifungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Sourthern Africa Telecom Association (SATA) kilichofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 za umoja huo zimeshiriki. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Waziri Kindamba.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 za umoja huo zimeshiriki Dkt. Ndugulile amezungumzia fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano hasa matumizi ya intanenti kuwa yanawezesha kufanyika kwa shughuli za biashara, uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Aidha amesema kuwa ni vema elimu ya matumizi sahihi ya mtandao iendelee kutolewa ili kupunguza uhalifu wa mitandaoni na mmomonyoko wa maadili kulingana na tamaduni zetu za kiafrika ambao kwa namna moja ama nyingine unasababishwa na kukua kwa matumizi ya intaneti.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (Katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Waziri Kindamba (kushoto) na Mhandisi Peter Ngaya wa Wizara hiyo wakisikiliza Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Sourthern Africa Telecom Association (SATA) kilichofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 za umoja huo zimeshiriki.

Dkt.Ndugulile amesema kuwa anatamani kuona gharama za mawasiliano baina ya nchi hizo za Afrika zinapungua kwa kutengeneza mfumo madhubuti wa kuwa na mawasiliano ya ndani ya Afrika (Regional Hub) badala ya kusafirishwa kwenda nchi za ulaya na marekani ndipo yarudi na kumfikia mlengwa.

“Serikali imewezesha kuwa na mawasiliano ya ndani kama nchi hivyo kushusha gharama za huduma za mawasiliano ambapo miongoni mwa zinazofanya vizuri sana kwenye huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu ni Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza katika bara la Afrika”, amezungumza Dkt. Ndugulile