December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndugulile: Tengenezeni maudhui ya elimu kwa njia ya intaneti

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira. Online

WAZIRI wa Mawasiliano, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wadau wa elimu kutengeneza maudhui ya elimu kwa njia ya mtandao, ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwasaidia kupata elimu bora.

Ngugulile aliyasema hayo katika ziara yake katika Ofisi ya Kampuni ya Shule Direct, inayotengeneza maudhui kwa njia ya mtandao hasa kwa elimu ya kwa wanafunzi nchini.

Alisema kwa utengenezaji wa maudhui kimtandao yanayoakisi maisha ya Watanzania, itasaidia kuifikisha elimu kwa ukaribu zaidi kwa vijana wa Kitanzania huku ikichagiza upatikanaji wa ajira kwa kuwa kazi ya kutengeneza maudhui, pia ni fursa ya kujiajiri.

Aliongeza kuwa licha ya Mtandao wa Intaneti, kufikia takribani asilimia 60 ya nchi nzima kwa kiwango cha 3G lakini, takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 28 pekee ya Watanzania ndiyo wanatumia huduma za intaneti kila siku tofauti inayoonesha kuwa pamoja na intaneti kuwepo, bado kuna gharama ya vifaa na data kuweza kutumia intaneti.

Ndugulile alisema serikali ipo kwenye mchakato wa kuendelea kutandaza mkongo wa taifa katika kila pande za Tanzania, kuhakikisha upatikanaji wa mtandao wa intaneti nchi nzima na kisha kuuza nchi za Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Alisema Wizara ya Mawasiliano kupitia taasisi zake, inaratibu mpango wa kugawa kompyuta zilizounganishwa na huduma za intaneti katika shule za sekondari, zinapatiwa ikiwa ni nyenzo ya kujifunzia na kufundishia shuleni.

“Tunaangalia upya mifumo ya ada na leseni mbalimbali zinazohitajika kufikia maudhui ya mtandaoni, nimeguswa na ubunifu mnaofanya Shule Direct hasa huyu Ticha Kidevu, mwalimu wa kwanza wa kidigiti nchini Tanzania, anayetumia majukwaa ya kidigiti ya kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema.

Waziri Ndugulile, atembelea Ofisi za Shule Direct na Ndoto Hub mkoani Dar es Salaam.

Shule Direct ni Shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa na kusimamiwa na vijana wa Kitanzania kwa lengo la kutumia teknolojia, kuwezesha upatikanaji wa nyenzo bora za kujifunzia na kufundishiwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

Naye mmoja wa Wakurugenzi wa Shule Direct, Rajabu Mgeni alisema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2013 mpaka sasa, watumiaji zaidi ya milioni tatu wameshatumia majukwaa hayo ya kidigiti ya Shule Direct, ambayo yanapatikana katika mifumo mbalimbali.

Rajabu alisema,” Shule Direct imemtengeneza mwalimu anayefundisha mtandaoni anayejulikana kwa jina la Ticha Kidevu ambaye kwa kupitia jukwaa maalum kwa wanafunzi wa Sekondari, Ticha Kidevu anafundisha masomo 13 ya kidato cha kwanza hadi cha nne kufuatana na mtaala wa Taifa wa elimu ya sekondari.”

Alisema mbali na mafanikio, lakini kuna changamoto zinazokwamisha azma ya Shule Direct la kuwafikia idadi kubwa zaidi ya watoto, ikiwemo gharama ya upatikanaji wa intaneti hali inayosababisha matumizi hafifu ya huduma za Shule Direct na hata huduma nyingine za elimu kwa njia ya mtandao.