December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndugai: Nisamehe… nisamehe, nimekosa mimi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dodoma

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusiana na kauli yake aliyodai alichezewa na mitandao ya kijamii na hakuwa na nia mbaya kama ambavyo imeeleweka.

Katika video hiyo, Spika Ndugai anaonekana akipinga utaratibu wa Serikali wa uchukuaji mikopo kutoka taasisi za fedha na kwamba kwa mwendo huo nchi itakuja kupigwa mnada.

Kufuatia video hiyo iliyozua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na kupewa uzito mkubwa na vyombo vya habari nchini, leo saa tano asubuhi, Spika Ndugai, amezungumza na waandishi wa habari na kumuomba radhi Rais Samia na wale wote waliokwazwa na kauli hiyo, kwani anatambua kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kipindi kifupi cha uongozi wake na kwamba yaliyofanyika kwenye Wilaya ya Kongwa hayajawahi kutokea.

Ametoa mfano wa mkopo wa sh. trilioni 1.3 ambazo Tanzania imepata kutoka IMF, akisema fedha hizo zimefanya mambo makubwa hasa katika Wilaya ya Kongwa ambayo imepata mgawo wa sh. bilioni 3 sawa na mapato yake ya ndani ya mwaka mmoja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.