January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndingo: Wananchi endeleeni kumsaidia,kumuombea Rais

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbarali

MBUNGE Mteule Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo amewataka wananchi wilayani humo kuendelea kumwombea Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na kumsaidia katika kuwaletea maendeleo.

Ndingo amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kata ya Kongolo Mswiswi kijiji cha Azimio Mapula wilayani humo.

Amewaomba wazee kuendelea kumwombea Rais Samia kwani ana nia ya dhati na njema kwa watu wa Kongolo Mswiswi na makundi yote ambapo mwaka huu mwezi Desemba watakuwa wamekamilisha zoezi la kufanikisha uratibu wa Bima za Afya kwa wazee wilayani humo .

Aidha ameeleza kuwa sera ya wazee inayotumika ni ya mwaka 2003 ambayo imepitwa na wakati ni muhimu kuhimiza serikali kufanya mapitio upya wa sera hiyo kisha ipelekwe Bungeni kwa ajili ya kutengenezewa sheria ili mambo ya wazee yawe katika sheria.

“Wazee ni watu muhimu sana katika Taifa hili ni kundi muhimu viongozi wa kitaifa wanapokuwa na jambo lolote gumu wanakaa nao,wanapofanya jambo kubwa lazima wakutane nao pia na wazee kwa hiyo,ndio maana tunasema wazee ni dawa na sisi Mbarali lazima tuhakikishe kundi hili muhimu kwenye jamii yetu linaendelea kuangaliwa kwa ukaribu,”amesema Mbunge huyo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Mbarali Mary Mbwilo amesema wazee ni tunu chama kinawathamini na kinawaelewa ndo maana muda wote wakiwa na jambo lolote wanawaita kwa msaada wa kimawazo kutokana na kujitambua kwao.

Aidha Mwenyekiti huyo alimshukuru Mbunge Bahati kwa upendo alioonesha kwa wazee kuwakatia bima ya afya.