Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amezihimiza Kamati za maafa nchini kuendelea kuweka mikakati Madhubuti katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Ameyasema hayo Mkoani Lindi alipokuwa akifungua kikao kazi cha kujenga uwezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa Mkoani humo kuhusu hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa kilichoratibiwa na Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kimelenga kuifikia mikoa katika kuzijengea uwezo kamati hizo katika ngazi zote.
Naibu Waziri huyo amezikumbusha Kamati hizo umuhimu wa kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kuzingatia madhara yatokanayo na maafa.
“Kikao kazi cha leo kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea,” alieleza.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wajibu wa kila mmoja katika eneo lake la kazi kuendelea kuchukua hatua stahiki endapo maafa yanatokea huku akieleza kuwa mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii yetu kutokana na matukio ya maafa.
“Uzoefu unaonesha kuwa kuchukua hatua za mapema za kuzuia na kupunguza madhara zimekuwa na gharama nafuu kuliko kusubiri ili kuchukua hatua baada ya maafa kutokea ambapo, serikali imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi, hivyo tuendelee kujipanga mapema,” alisisitiza
Mhe. Nderiananga alikumbusha kuwa hatua hii ni muhimu ili kuhakikisha juhudi zinazochukuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha uchumi na huduma za kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa.
“Ni dhahiri kuwa hatua mnazochukua zitachangia katika juhudi zake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali pamoja na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 kwa manufaa makubwa kwa wananchi na tija iliyokusudiwa,” alisema Naibu Waziri huyo.
Akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe Shaibu Ndemanga amesema mkoa umeendelea na jitihada za kujiandaa na madhara yanayoweza kutokea kutokana na maafa huku ikiendeelea kujipanga na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kwa kuzingatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya uwepo wa Mvua za El nino na kuahidi kutekeleza maagizo na maelekezo yaliyotolewa kwa kuzingatia umuhimu wa tahadhari za mapema.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu