Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema mradi wa kimkakati wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga nchini Tanzania wa EACOP (East African Crude Oil Pipeline), umefikia asilimia 86 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2026.
Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo, Juni 29, 2026, wakati akikagua utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika eneo la Chongoleani, mkoani Tanga.
Ndejembi amesema kuwa kutokana na kasi nzuri ya utekelezaji wa mradi huo, meli ya kwanza inatarajiwa kuchukua mafuta ghafi kutoka Chongoleani mwezi Januari 2027, hatua muhimu inayosubiriwa kwa hamu.

Akitoa maelekezo kuhusu changamoto zilizobainishwa na mkandarasi, Waziri Ndejembi amemtaka mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa njia ya umeme itakayotumika katika uendeshaji wa mitambo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ifikapo mwanzoni mwa mwezi Agosti.
“Changamoto ndogo ndogo tulizozikuta ni kama umeme bado line hazijafika na nimemtaka mkandarasi kupitia Shirika letu la TANESCO kuhakikisha mpaka ifikapo tarehe ya mwisho wa mkataba wake awe amekamilisha kazi yake,” amesisitiza Waziri Ndejembi.

Amesema mradi huu ni miongoni mwa miradi ya mfano nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, ukiwa umegharimu Dola za Marekani Bilioni 6.02. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechangia Dola za Marekani Milioni 374, sawa na asilimia 15 ya mchango wa wanahisa.
Kadhalika, Waziri Ndejembi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia vizuri na kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi huo. Amesema katika kipindi cha ujenzi, jumla ya ajira 10,000 zimezalishwa, ambapo ajira 7,500 sawa na asilimia 75 zimenufaisha Watanzania.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo nchini Tanzania kwa ushirikiano na Uganda.
Amesema kati ya mikoa nane inayopitiwa na mradi huo, Mkoa wa Tanga umefaidika kwa kiwango kikubwa kupitia fursa mbalimbali za ajira na maendeleo kwa wananchi, hususan vijana.


More Stories
Nmb yazindua kadi inayorahisisha upatikanaji wa mitaji
Pedima ang’ara kimataifa,Tuzo za Ubunifu
Wakulima Mil. 1.3 kunufaika na teknolojia ya kidigitali