




i
Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Tanzania imeingia katika hatua mpya ya matumizi yenye tija ya umeme kwa kuzindua mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme kwa wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, hatua inayolenga kupunguza gharama za maisha, kulinda mazingira na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Akizungumza Juni 11,2026 jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ukopeshaji wa majiko ya umeme kwa wateja wa TANESCO na uzinduzi wa mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, Ndejembi alisema miradi hiyo miwili ni ushahidi wa namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza kwa vitendo agenda ya matumizi ya nishati safi nchini.
Amesema Tanzania sasa ina umeme wa kutosha kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo uzalishaji wa umeme umefikia zaidi ya megawati 4,000, huku kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kukiimarisha zaidi uhakika wa nishati nchini.
“Tumetoka kwenye hatua ya kuhakikisha umeme unapatikana, sasa tunaelekea kwenye hatua ya kuhakikisha umeme huo unawanufaisha wananchi moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku,hii ndiyo maana ya maendeleo ya kweli na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Ndejembi.
Kuhusu mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme, Waziri huyo amesema unatekeleza moja kwa moja malengo ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku asilimia 20 wakitumia umeme kupikia.
Ameeleza kuwa kupitia mfumo wa ‘On-Bill Financing’, wananchi watapata majiko ya umeme kwa mkopo na kurejesha gharama zake kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU, hatua itakayosaidia kuondoa kikwazo cha gharama za awali za ununuzi wa majiko hayo.
“Ninafurahi kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kutekeleza mfumo huu kwa vitendo. Tunamwondolea mwananchi kikwazo kikubwa kilichokuwa kinamzuia kuingia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme,” amesema.
Aidha, amesema matumizi ya umeme katika kupikia yatachangia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umeendelea kusababisha uharibifu wa mazingira, huku zaidi ya hekta 469,000 za misitu zikipotea kila mwaka kutokana na matumizi hayo.
Ndejembi amesema faida nyingine za kupikia kwa umeme ni pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya nishati majumbani, kulinda afya za wananchi dhidi ya magonjwa yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa pamoja na kuokoa maisha ya wanawake na watoto wanaokumbwa na athari za matumizi ya nishati zisizo safi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amezindua rasmi mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, akisema Tanzania imeamua kuwa sehemu ya mapinduzi ya uchumi wa kijani yanayoendelea duniani badala ya kubaki mtazamaji.
Amesema ongezeko la matumizi ya magari, pikipiki na bajaji zinazotumia umeme nchini linaonesha wananchi wameanza kutambua faida za teknolojia hiyo kutokana na gharama ndogo za uendeshaji na urafiki wake kwa mazingira.
Kwa mujibu wa Ndejembi, changamoto kubwa iliyokuwa imebaki ni upatikanaji wa miundombinu ya kuchajia vyombo hivyo, jambo ambalo sasa linaanza kupatiwa ufumbuzi kupitia mradi huo utakaohusisha ufungaji wa mashine 50 za kisasa za kuchajia magari ya umeme katika ofisi za TANESCO za mikoa yote nchini.
Ameema mradi huo umefanikishwa kwa ushirikiano wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na kampuni ya AUTEL, ambayo imechangia upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.
“Ninawahakikishia Watanzania kwamba ukinunua gari la umeme leo usiwe na wasiwasi wa kusafiri ndani ya nchi. TANESCO imeanza kujenga mtandao wa kitaifa wa vituo vya kuchajia utakaorahisisha matumizi ya teknolojia hii,” amesma.
Katika maelekezo yake kwa TANESCO, Waziri Ndejembi aliitaka taasisi hiyo kuhakikisha mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme unawafikia wananchi wa maeneo yote nchini, kuongeza elimu kuhusu matumizi ya umeme kupikia na kukamilisha kwa wakati ujenzi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.
Pia aliagiza Wizara ya Nishati kupewa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo kila baada ya robo mwaka ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Amewataka wananchi kutumia fursa ya mikopo ya majiko ya umeme yenye masharti nafuu pamoja na huduma ya kuchaji bure kwa siku 30 za mwanzo katika vituo vipya vya TANESCO kabla ya kuanza kwa utozaji wa gharama nafuu zitakazowekwa baadaye.
Aidha Ndejembi a.eipongeza TANESCO kwa kuendelea kubuni miradi inayowaletea wananchi manufaa ya moja kwa moja na kusema historia ya mapinduzi ya nishati safi nchini itakumbuka kuwa safari hiyo haikuanzia kwenye vituo vya kuzalisha umeme pekee bali ilianza kwa kupeleka umeme jikoni na barabarani kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange amesema Shirika hilo lipo kwenye safari ya mapinduzi ya nishati safi katika kifikia malengo ya kihakikisha wamefikia wateja milioni moja katika kilindi cha miaka mitatu.
Aidha ametoa ofa kwa wote wenye vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme kujaza nishati hiyo bure kwa kipindi cha mwezi mzima katika kituo kilichozinduliwa leo katika ofisi ya TENESCO mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya Nishati hiyo

More Stories
FCC,ZFCT zaimarisha ushirikiano
Mha.Mramba akutana na wadau wa Kimataifa kuharakisha miradi ya Jotoardhi
Wakulima wa pamba wafungua akaunti kwa wingi