April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi aitaka Takukuru kusimamia Fedha za IMF

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

NAIBU Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora,Deogratius Ndejembi imeiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU),kuwa wakali katika  kufuatilia na kusimamia fedha zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule na vituo vya afya.

Ndejembi amesema hayo jijini hapa,wakati akifunga Mkutano Mkuu wa mwaka wa wakuu wa TAKUKURU ambapo alisema kuwa kuna viashiria vya rushwa katika fedha hizo  huku akidai kuna maeneo tofali linafuatwa umbali wa kilomita 150 wakati kuna uwezekano wa kupatikana kwa urahisi

“Rais Samia  amezindua Mpango wa Serikali  kuinua uchumi na kukabilina na ugonjwa wa virusi vya Corona kwa kutumia mkopo wa fedha wa shilingi Trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kutoa onyo Kwa watendaji  kuzielekeza fedha hizo kwenye malengo yaliyokusudiwa hivyo lazima tufate maelekezo hayo,”amesema.

Hata hivyo Ndejembi, amekosoa uamuzi wa baadhi ya watendaji kuchukua muda mrefu kwenye ushindani wa zabuni na kushindwa kukidhi mahitaji muhimu ya muda wa utekelezaji wa miradi ndani ya miezi tisa kuanzia sasa na kubainisha kuwa  hali hiyo huenda ikawa ni kiini cha rushwa, uzembe, upendeleo, pamoja na uwezo mdogo wa mzabuni.

“Nawaagiza TAKUKURU nendeni mkasimamie fedha za miradi zilizotolewa na Rais, kuna viashiria vya rushwa katika fedha hizo ,maeneo mengine tofali linafuatwa umbali wa kilomita 150 mtu mmoja anapewa tenda za kununua matofali,kuna maeneo mengi ujenzi  umesimama ukiuliza unaambiwa nondo zimeisha,hapa kuna viashiria vya rushwa,niwaombe sana mfuatile na muwe wakali,”amesema.

Vilevile,Naibu waziri huyo  ameitaka TAKUKURU kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwa na mipango ya katika kuzuia zaidi ili kuleta faida.

“Tusimame imara tuwadhibiti watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea  simamieni rushwa na mmomonyoko wa maadili huku mkizingatia utoaji wa haki,”amesema.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mkuu  wa TAKUKURU,Kamishna wa Polisi  Salumu Rashid  Hamduni,amesema katika Mkutano huo wa siku tatu uliohusisha  viongozi  wa Taasisi hiyo kutoka mikoa  28 wameweza kutathmini utendaji  wao na kujadili namna Bora ya kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa.

“Kwa muda wa siku tatu tumejifunza mengi kupitia mada mbalimbali za misingi ya maadili na mashauri ya kinidhamu,yote haya ni kuhakikisha chombo hiki kinakuwa cha mfano, kwa ujumla kila mmoja wetu amépata tiba anayostahili,”amesema Hamduni.

Pia amesema  Taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti kubaini njia bora za kuziba mianya ya rushwa na kwamba kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla  ya shilingi billioni 29.3 ziliokolewa na kwamba  billion 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslim  na utaifishaji mali huku kiasi cha  bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.

Ameeleza kuwa miradi ya kimaendeleo 1,188 yenye thamani ya billion 714.17 katika sekta ya  afya maji elimu  ziliweza kufatiliwa na kuona makosa  ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumejifunza namna ya kudhibiti hisia hasi na mahusiano kazini,hali hii itatupa nguvu zaidi ya kuzuia vitendo vya rushwa na kuongeza kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watuhumiwa Mahakami kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya  mashtaka ,”amefafanua

Pamoja na hayo ameleza kuwa jumla ya majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa huku majadala  339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi  wa mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakani esi mpya  zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345.