May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NDC yaikumbuka CSP Siku ya Wanawake Duniani

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Dar

SHIRIKA la Taifa la Maendeleo (NDC), Leo Machi 8, 2024 ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, limeadhimisha kwa kushiriki katika zoezi la unyunyiziaji dawa wa mashamba ya mbogamboga, yanayolimwa na kikundi cha Cooperative Small Peasant kilichopo Mpiji Magohe Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa zoezi hilo la unyunyizi wa dawa, Mratibu wa zoezi hilo wa NDC, Esther Mwaigomole, amesema zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kutambua jitihada zinazofanywa na wanawake wa NDC za kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wakulima, lakini pia kutumia nafasi hiyo kuitambulisha dawa mpya kwa wakulima maarufu kama Thursave 24.

Huku akisema kuwa, ujio huo utawasaidia wakulima katika kuwahakikishia usalama wa chakula pamoja na kuachana na matumizi ya dawa zenye kemikali ambazo zina athari kubwa kwa afya za watumiaji wa mazao yao.

” Wanawake wa NDC leo tumeungana na Hawa wakulima na tunawashauri waendelee kuitumia dawa hii kuanzia sasa na siku zijazo ili kuwahakikishia usalama na afya zao kwakuwa ni dawa ya viuatilifu hai na haina kemikali ya aina yoyote ikilinganishwa na aina nyingine za dawa”, amesema Mwaigomole.

Aidha kwa upande wake, Mwakilishi kutoka kiwanda kinachozalisha dawa za Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) Cha Kibaha Mkoani Pwani, Jovin Magaine, Amesema TBPL ni mali ya Serikali na kinamilikiwa kupitia NDC, ambapo nia yake ni kuhakikisha inawasaidia wananchi katika katika kuboresha afya zao kupitia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kiwandani hapo.

Pia amesema, katika awamu ya kwanza kilianza na uzalishaji wa bidhaa za viuadudu ambayo ni mahususi katika Kupambana na Malaria hapa nchini na sasa kimeamua kuanzisha usambazaji wa viuatilifu hai kwa ajili ya kupambana na wadudu dhurifu katika kilimo ikiwa ni moja kati ya changamoto inayowakabili wakulima wengi nchini.

Nao baadhi ya wanachama wanaounda kikundi cha Cooperative Small Peasant, wamelishukuru Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Kiwanda cha TBPL kwa kuwakumbuka na kushirikiana nao katika zoezi la unyunyizi na kudai kuwa uwepo wa wadudu dhurifu katika mbogamboga limekuwa ni tatizo sugu na kuamini kuwa ujio wa dawa hiyo utaenda kulimaliza.

” Tunaishukuru sana NDC kwani dawa hii umekuwa wakati sahihi kwani tatizo la wadudu dhurifu katika mazao yetu limekuwa la muda mrefu na kwa ujio wa dawa hii mpya tunaamini tunakuwa tumepata mkombozi”, amesema Abdallah Said mmoja wa wakulima aliyeshiriki katika zoezi hilo.