Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua Chuo cha Ufundi Stadi Nyamidaho kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma huku akisema kuanzishwa kwa chuo hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga vyuo hivyo katika kila wilaya nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa chuo hicho, Profesa Ndalichako amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma hiyo ya vyuo vya ufundi stadi inakuwa karibu na wananchi na kuwawezesha kupata ujuzi wa aina mbalimbali na kujikwamua katika umasikini wa kipato.
Ndalichako amesema Chuo cha Nyamidaho kimetokana na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Taasisi ya World Vision ambapo Serikali imekarabati majengo yaliyokuwepo na kujenga mengine mapya.
Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako jumla ya shilingi milioni 534 zilitolewa kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba zimetumika milioni 477 hadi ukamilishaji. Aidha ameridhia ombi la kiasi kilichobaki kutumika kuanzisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume.
Ndalichako amesema, katika mwaka 2019/20 vyuo 10 vya halmashauri za wilaya vimejengwa na kuanza kutoa mafunzo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kukamilisha ujenzi wa chuo hicho na amewataka wakazi wa Kijiji cha Nyamidaho kuhakikisha vijana wao hasa wa kike wanajiunga na chuo hicho.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki ameishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha elimu ya ufundi nchini huku akisema kuwa Chuo hicho kipya kina wanafunzi takriban 70.
Maduki ametumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa VETA kutoa bure mafunzo ya kozi ya uwashi kwa wanafunzi wanaotoka Nyamidaho.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano