October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndairagije: Tutaendelea pale tulipoachia

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Etienne Ndayiragije amesema kikosi chake kitaendelea pale walipoishia katika mchezo wao wa nyumbani wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) dhidi ya Tunisia.

Tanzania itaingia katika mchezo huo wa marudiano wa Kundi J utakaochezwa Novemba 17 katika uwanja wa Benjamin Mkapa kusaka alama tatu baada ya kukubali kipigo cha goli 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Novemba 13 katika uwanja wa Stade Olmpique de Rades uliopi Tunis.

Goli pekee katika mchezo huo lilifungwa dakika ya 18 kwa la mkwaju wa penati na Nahodha Youssef Msakni baada ya golikipa wa Tanzania Aishi Manula kumchezea madhambi ndani ya eneo la 18 alipokuwa akijaribu kuokoa mpira.

Kocha huyo amesema kuwa, kilichowakwamisha ni makosa madogo madogo yaliyofanywa na wachezaji wake ikiwemo kutojiamini katika dakika za mwanzoni.

Lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo wachezaji wake waliporudi mchezoni na kuanza kujiamini hivyo anaimani kuwa watakwenda kuanzia pale walipoishia na kupindua matokeo hayo waliyoyapata ugenini.

Kocha huyo amesema kuwa, kwa sasa moja kwa moja wanaanza mazoezi kuelekea kwenye mchezo huo utakaochezwa kesho bila kujali kuwa wamechoshwa na safari.

“Ni mweli wachezaji wamechoka kwani hawajapata muda wa kupumzika lakini kama timu tumeamua kuwa tunakwenda kubeba bendera ya Taifa hivyo ni lazima kujitoa kwa hali na mali ili kufikia malengo yetu, ” amesema Ndayiragije.

Pia kocha huyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo ili kuwapa sapoti na hamasa wachezaji kwani uwepo wao ndio utakaochangia timu yao kushinda nyumbani.

“Tunawaomba mashabiki kuja kutuunga mkono licha ya kuwa mchezo wetu utachezwa usiku kwani uwepo wao ni muhimu sana, tutajitoa na tutapambana kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunajipambana kuchukua ushindi,” amesema kocha huyo.

Katika Kundi, Taifa Stars wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi tatu sawa na Libya na Equatorial Guinnea huku Tuminia akiongoza kundi hilo akiwa na alama tisa baada ya kushinda mechi zake zote tatu.