Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
TANZANIA imeendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa katika sekta ya biashara ya kaboni, kufuatia kampuni ya Carbon Bridge kueleza nia ya kupanua uwekezaji wake nchini kupitia miradi ya kimkakati inayolenga kuzalisha viwango vya kaboni (Carbon Credits).
Nia hiyo imeelezwa katika mazungumzo kati ya kampuni hiyo na wataalamu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaoendelea jijini Antalya, Uturuki.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Novemba 11, 2026, Carbon Bridge imeeleza kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini, fursa zilizopo katika sekta mbalimbali pamoja na mfumo wa uratibu na usimamizi wa biashara ya kaboni unaosimamiwa na Serikali kupitia NCMC.
Kampuni hiyo imeonesha nia ya kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya biashara ya kaboni, ikitambua uwezekano wa Tanzania kuzalisha viwango vikubwa vya kaboni kupitia rasilimali na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi.

Ushiriki wa NCMC katika mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuitangaza Tanzania kama eneo lenye mvuto kwa uwekezaji wa biashara ya kaboni, kuimarisha ushirikiano na wawekezaji wa kimataifa na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa tija kupitia uwekezaji wenye uadilifu na manufaa kwa taifa.
Ujumbe wa NCMC katika mazungumzo hayo uliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji, Usajili na Utoaji Taarifa za Miradi, Dkt. Deo Shirima, akifuatana na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Mazingira, Ushauri na Utafiti, Dkt. Paul Lyimo; Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Risper Koyi; pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ibrahim Hamidu.

Kwa upande wa Carbon Bridge, ujumbe wake ulijumuisha Afisa Mtendaji Mkuu, Marion Verles; Afisa Mkuu wa Masuala ya Kaboni, Donee Alexander; na Mkurugenzi wa Sera na Maendeleo ya Biashara, Fabio Marque.



More Stories
Dkt.Mwigulu mgeni rasmi kilele miaka 40 COSTECH
Wananchi waunganisha nguvu Watoto wapate chakula shuleni
Homera ampongeza Rais Samia kwa ajenda ya nishati safi