
Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Chunya
UONGOZI wa Kata ya Lualaje, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, umesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano kimejipanga kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha maeneo korofi ya barabara yanakarabatiwa ili ziweze kupitika wakati wote, ikiwemo kipindi cha mvua.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila kukumbwa na changamoto za kukatika kwa mawasiliano kutokana na ubovu wa barabara.
Akizungumza na Timesmajira kuhusu mikakati ya kuboresha miundombinu hiyo, Diwani wa Kata ya Lualaje, Leckson Mwakasuluka, amesema barabara ni miongoni mwa vipaumbele vya uongozi wa kata hiyo kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya wananchi.

Amesema barabara ya Lualaje inayopakana na Kata ya Lupa imekuwa na changamoto ya kupitika wakati wa mvua, hali inayosababisha mawasiliano kukatika katika baadhi ya maeneo.
“Barabara ya Lualaje inayopakana na Lupa ina maeneo ambayo mvua zinaponyesha mawasiliano hukatika. Hivyo, kama viongozi tumekubaliana kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote.
“Katika kutekeleza azma hiyo, tunashirikiana na TARURA pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, ambayo tayari ina mitambo ya ujenzi wa barabara. Vilevile, wananchi wamekuwa tayari kujitolea kuchangia mafuta kwa ajili ya kurekebisha baadhi ya maeneo,” amesema Mwakasuluka.
Aidha, amesema katika msimu huu TARURA imetenga kilomita 23 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika kata hiyo, ambapo utekelezaji wake utazingatia zaidi maeneo korofi yenye uhitaji mkubwa.
Amesema pamoja na kuwa baadhi ya barabara zinaweza kupitika bila kufanyiwa matengenezo, uongozi wa kata utahakikisha kilomita hizo 23 zinatumika katika maeneo ambayo ubovu wake unaweza kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Lualaje na kata nyingine.
Mwakasuluka amebainisha kuwa kukatika kwa barabara kunaathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, zikiwemo usafirishaji wa mazao ya wakulima, upatikanaji wa huduma za afya na elimu.
Amesema uongozi wa kata umejipanga kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa matengenezo hayo ili kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na wananchi wanapata uhakika wa usafiri na mawasiliano wakati wote.


More Stories
Ndejembi ataka mradi wa umeme songea-masasi ukamilike
Wakulima Ruvuma kunufaika na mfumo wa stakabadhi za ghala
TANAPA kukabidhiwa msitu wa burka kuimarisha uhifadhi wa mazingira