Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Arusha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mwanamke shupavu na tunu kwa Taifa, hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi zake za kuiletea nch maendeleo.
Dkt. Nchimbi amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kilombero jijini Arusha leo Juni 3, 2024.
“Kazi zilizofanywa na Rais Samia katika miaka mitatu ni nyingi na kila mbunge amezungumza kwa kujiamini kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa majimboni mwao na hakuna kipindi kilicholetwa fedha nyingi za maendeleo kama Cha awamu hii ya Dkt.Samia.”amesema Balozi Dkt.Nchimbi na kuongeza kuwa
“Hakuna katika historia yetu kipindi ambacho vituo vya afya, hospitali, vifaa tiba, madarasa, shule, barabara, miradi mikubwa ya kimkakati imeendelezwa na kujengwa kama wakati huu wa Rais Dk Samia,”
Amesema, katika mazingira hayo hakuna atakayesema serikali ya Rais Samia haijafanya kazi nzuri iliyotukuka.
Kuhusu maandamano ya wapinzani, amesema kuwa wapo baadhi ya wanaCCM na wananchi walikerwa na maandamano.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amesema, Arusha ni ngome ya CCM kwani wanachama na wananchi wanakiunga mkono.
Alibainisha kuwa, kasi ya maendeleo inaonekana, hivyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa kura zote kwa wagombea wa CCM.
Amesema, Arusha imetulia, siyo ya zamani ya watu kuandamana, watalii wanaonekana, maendeleo yanaonekana msirudi nyuma. Kuandamana ni uzururaji kama uzururaji mwingine na kumshauri mchungaji Msigwa kujiunga na CCM na kusema kuwa ndiyo chama chenye demokrasia ya kweli.
“Wenzetu wanamgogoro mkubwa, hakukaliki. Wanaleta ubaguzi ni msongo wa mawazo,” alisisitiza.
Katibu wa NEC, Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Himid, amesema ziara za Rais Dk. Samia zinamanufaa kwani akiwa nchini Korea amepata sh. trilioni sita za maendeleo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema watendaji wa serikali katika mkoa huo wasiotimiza majukumu yao, atahakikisha anawawajibisha hadi wakae sawa na hiyo yote ni kwa manufaa ya wananchi.
Amesema mkoa huo unaongozwa na utalii, biashara na usafirishaji, hivyo amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutangaza vivutio vilivyopo katika mkoa huo.
“Nimekuta mkoa una changamoto ya uwepo wa watumishi wasiokuwa wazalendo, wenye kutanguliza maslahi yao binafsi.
“Naomba ukaniombee nivumiliwe kidogo nisihamishwe katika Mkoa huu mpaka wale watendaji wasiotimiza majukumu yao ipasavyo wale “spana” za kutosha hadi wanyooke na mpaka tarehe 1, 2025 mkoa huu utakuwa wa kwanza kwa kila kitu,” amebainisha.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini (CCM) Mrisho Gambo, amesema jimbo hilo limepata mradi wa Benki ya Dunia ambao utajenga barabara za lami.
Pia, amesema kupitia mradi huo litajengwa soko kubwa la kisasa kwa Mromboo, Kilombelo pamoja na kituo kipya cha mabasi.
Ameeleza kuwa, Rais Samia amejenga barabara za lami Elboro, Kijenge, Muriet na barabara ya Mianzini – Ngaramtoni – Mianzini.
“Dk. Samia ametujengea shule mpya tano za sekondari, upande wa afya Hospitali ya Mount Mero wamepewa X-Ray ya kisasa na CT-Scan.
“Kubwa zaidi mwaka 2020 kilio kikubwa kilikuwa shughuli za utalii, lakini tangu alipoingia Rais Samia kila siku mikutano inafanyika, shughuli za utalii na ujasiriamali zimefunguka,” alibainisha.
Hata hivyo, amebainisha kwamba, kuna changamoto kama Rais Dk. Samia analeta miradi lakini wasimamizi wanalegalega, Chama kitapata hasara.
Amebainisha kuwa madini ya Tanzanite yanazuiwa, hayauzwi Arusha na kusababisha watu kukosa ajira.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua