December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NCD inaongeza mzigo huduma za afya nchini

Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) Neema Lugangira ameitahadharisha jamii kwa kuitaka iwe makini dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) kwa kile alicholeza kuwa yanaongeza mzigo kwenye mfumo wa utoaji huduma za afya nchini.

Hali hiyo ameielezea kuwa ina changamoto nyingi za kiuchumi kwa jamii na taifa kwa sababu NCD hutibiwa kwa muda mrefu na dawa zake ni za gharama kubwa.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanavyoongezeka na yanaongeza mzigo kwenye mfumo wa utoaji huduma za afya na hata kwenye uchumi wa taifa,” alisema Lugangira kwenye mkutano wa wadau wa NCD aliokuwa amealikwa kama mgeni rasmi.

Kutokana na hali hiyo aliwataka wahudumu wa afya nchini, wadau wa NCD na vyombo vya habari kuwekeza nguvu katika kuelimisha jamii ili iepuke magonjwa haya ambayo kasi yake inaongezeka kwa kasi.

Baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya mfumo wa hewa na shinikizo la damu.

Ameitaka Serikali pia kuchukua hatua ya kudhibiti bidhaa ambazo zinachangia kasi ya magonjwa hayo nchini kama vile tumbaku, pombe na vinywaji vyenye suka nyingi vinavyosindikwa viwandani.

mazoezi ambayo ni sehemu muhimu kwa afya ya binadamu

“Kuna tatizo la kuwalinda watumiaji bidhaa, utakuta juisi boksi linaonyesha kuwa ya matunda halisi, lakini kumbe ni sukari, rangi na ladha tu.

“Hakuna wa kuyasemea, hayo huchangia tutafute namna kuyasemea hayo tuokoe watu,” alionya mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kupambana na NCD, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Omary Ubuguyu alibainisha maeneo mbalimbali yenye upungufu katika kupambana na magonjwa hayo nchini.

Ameyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na kiwango hafifu cha uongozi, ushirikishaji pamoja na kukosekan kwa mpangilio kwenye baadhi ya mambo ikiwamo utoaji mafunzo.

“Kiwango kidogo cha watumishi na watoa huduma za NCD ambacho sasa ni asilimia 46 tu,” alisema huku akitaja kasoro nyingine ni ukosefu wa fedha na huduma thabiti za dharura katika tiba.

“Utafiti uliofanyika mwaka 2017 unaonesha upungufu wa watumishi kwa asilimia 54. Si hivyo tu bali pia huduma kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza zipo chini, mfano utafiti huo unaonyesha wagonjwa wa kisukari waliopatiwa huduma ni asilimia 30 na saratani ni asilimia nne pekee.”

Katika mkutano huo ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wa NCD walikubaliana kuwekwa mikakakati madhubuti ya kuboresha hudma kwa magonjwa hayo nchini na asasi zote za NCD ziwasilishe serikalini mikakakti yake.