Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC)limesema limeendelea kuratibu utatuzi wa migogoro ya miradi ya ujenzi ambapo jumla ya mashauri sita yametolewa uamuzi huku mengine 31 yakiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 13,2023 na Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo,Dkt.Matiko Mturi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya baraza hilo.
Dkt.Mturi amesema kuwa wanatatua migogoro hiyo ikiwa ni sehemu ya majukumu yao kama baraza linaloshughulika na sekta ya ujenzi.
“Baraza la Taifa la ujenzi linatoa huduma mbalimbali kwa wadau wa sekta ya ujenzi ikiwemo uratibu wa sekta,ushauri wa masuala yoyote yanayohusu sekta ya ujenzi,uratibu wa usuluhishi wa migogoro katika sekta ya ujenzi,
“Kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta ya ujenzi,ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya ujenzi,utafiti,ukusanyaji,uchapishaji na usambazaji wa taarifa za sekta ya ujenzi na miongozo mbalimbali ya gharama za ujenzi nchini,”amefafanua Dkt.Mturi.
Dkt.Mturi ameeleza kuwa kutokana na majukumu hayo wanayoshughulika nayo katika kipindi cha Julai 1,2022 hadi Januari 31, 2023 NCC imefanikiwa kutekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kuandaa rasimu ya mapendekezo ya gharama za msingi za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na kuwakilisha katika kikao cha wadau wa ndani ya serikali ili kupata maoni na ushauri wao.
Pia ameeleza mipango ya utekelezaji kwa Februari 1, 2023 hadi Juni 30 ,2023 kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kusimamia mikataba ya ujenzi kwa wadau wa sekta ya ujenzi hususan taasisi za umma zinazotekeleza miradi ya Miundombinu.
Pamoja na hayo Dkt.Mturi ameeleza kuwa lilihamasisha uundwaji wa bodi za usajili na vyama vya wadau wa sekta ya ujenzi likiwa na lengo la kutoa fursa kwa wataalam katika sekta ya ujenzi kutekeleza kazi zao kwa kuongozwa na mifumo iliyowekwa na Serikali pamoja na kulinda taaluma katika sekta hiyo.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili