April 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NCAA:Filamu za ‘Royal Tour’,Amaizing Tanzania zimechangia ongezeko la watalii Ngorongoro

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro(NCAA) imesema takwimu zinazoonesha kuwa juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu za Royal Tour na Amaizing Tanzania zimechangia kutangaza nchi na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio  vya utalii nchini.

Ambapo katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2025 , watalii wapatao milioni 2.9 wametembelea vivutio vya utalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 10,2025 na Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya  Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Dkt.Elirehema Doriye wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na muelekeo wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Dkt.Elirehema amesema kuwa katika kipindi hicho mapato ya shilingi bilioni 693.959 yamekusanywa  na kuingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kwa Mujibu wa Mkurugenzi  huyo ,katika mwaka 2024/2025 ,mwenendo unaonesha  Mamlaka itapata watalii zaidi ya milioni Moja na mapato zaidi ya lengo ambalo iliweka lankukusanya shilingi bilioni 230  huku akisema Hadi sasa wameshakusanya asilimia 92 ya lengo.

Aidha amesema mikakati mbalimbali ya Shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta Binafsi na Mamlaka za utalii umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hili la watalii.

“Katika jitihada za kuboresha huduma za utalii ,Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na kuboresha barabara ndani ya Hifadhi ,kuimarisha viwanja vya ndege vya ndani ya Hifadhi,kuboresha kambi za wageni ,kuimarisha Mifumo ya malipo,kuimarisha ulinzi Usalama wa wageni  na kuboresha vyoo vya wageni,”amesema Dkt.Elirehema.

Akizungumzia suala la kuhama kwa hiari ndani ya Hifadhi,Dkt.Elirehema amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi ya 2022,kumekuwa na ongezeko la watu na mifugo huku akisema wakati Hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 ,idadi ya wakazi ilikuwa takriban 8,000 ambapo wakazi 4,000 tayari walikuwa ndani ya Hifadhi na 4,000 walihamia Kutoka Hifadhi ya Serengeti na kwamba mifugo iliyokuwepo ilikadiriwa kufikia 260,000.

“Hata hivyo idadi ya watu na mifugo imeongezeka  kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni ambapo kwa mujibu wa sensa ya 2022 takwimu zinaonesha kuwa idadi imeongezeka Kutoka 261,000 Hadi zaidi ya 850,000 huku eneo la Hifadhi lokibaki na ukubwa ule ule wa kilometa za mraba 8,292 pekee,”amesema Dkt.Elirehema.

Ameeleza kuwa kutokana na ongezeko hilo la watu na mifugo kumekuwa na changamoto kubwa katika uhifadhi na ustawi wa wakazi wa Ngorongoro huku akisema ili kuboresha maisha ya wananchi ni kuwaondoa katika hatari ya kuishi pamoja na wanyamapori.

“Mwaka 2021 Serikali ilianzisha mradi wa kuwahamisha wananchi kuhama kwa hiari Kutoka Ngorongoro kwenda Kijiji Cha Msomera wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

“Tangu Juni 2022 lilipoanza zoezi la kuhamasisha wananchi kuhama kwa hiari kwenda Msomera,hadi disemba 2024 maendeleo mbalimbali yamepatikana ikiwemo kaya 1,678 zenye jumla ya watu 10,073 na mifugo 40,593 tayari wameshahama Kutoka Ngorongoro kwenda  Msomera.

Aidha amesema nyumba 3,003 zimejengwa kwa ajili ya Makazi ya wakazi wanaohamia Msomera  ambapo nyumba 1,495 zimekwishakaliwa na wananchi  waliokwiahahama na nyumba 1,508 ziko tayari kwa ajili ya wananchi wengine wakisubiri  kukamilika kwa miundombinu ya kijamii.