May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBS watakiwa kuwa wavumilivu wawapo kazini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

NAIBU Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Hamad Hassan Chande amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuwa waadilifu na waaminifu katika mchakato mzima wa uzalishaji wa Takwimu kuanzia kukusanya data, kuchakata data, kutafsiri data na utoaji wa taarifa. 

Amesema ili wawezekupanga mipango mizuri ya maendeleo wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa kuwa kazi za takwimu ni ngumu, zinahitaji muda na akili iliyotulia, hivyo wavumilie kidogo wanachokipata kwa maslahi mapana ya Taifa letu bila kulitia Taifa katika hasara.

Chande amesema hayo jijini hapa leo Mei 3,2023 wakati akifungua mkutano wa wafanyakazi hao ambao amesema ili kufikia malengo na kutekeleza adhma ya serikali ni muhimu kujiandaa kufanya kazi kwa kujituma na kwa kuzingatia weledi na umoja nia ni kuhakikisha wanafikia malengo katika kazi zao. 

“Ili kuongeza ujuzi kila mara fursa inapopatikana wa ndani ya nchi na nje ya nchi, nchi yetu bado ina mahitaji makubwa sana ya kitakwimu hususan za hali ya umaskini wa watu wetu ili kujua namna bora ya kuondoa umaskini katika ngazi zote za kijamii,

“Serikali inatambua umuhimu wenu na ndio maana inapitia upya maslahi yenu ili muweze kufanya kazi kwa maslahi ya taifa na ikitokea fursa ya kwenda kuongeza ujuzi nenda kwa sababu ukiongeza maarifa naamini kuwa hata utendaji kazi utaongezeka na utakuwa na ufanisi mkubwa,”amesema Chande

Aidha amesema kuwa  Serikali itahakikisha kuwa itatumia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa mafanikio makubwa ikiwemo kupanga na kupeleka miradi ya maendeleo kwa usawa kulingana na idadi ya watu wanaopatikana kwa eneo husika.

“Serikali haipo tayari kuona gharama kubwa zilizotumika kuandaa na kuendesha zoezi la Sensa ya watu na makazi lililofanyika 2022 zinapotea bure ni lazima Matokeo yale yatuletee faida chanya,”amesisitiza Chande

Naye Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Anne Makinda, amesisitiza kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kutumia maarifa waliyoyapata katika kuwaletea wananchi maendeleo kwani matokeo hayo ndio mlango wa serikali katika kufanya maendeleo

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa NBS imeendelea kufanya mapinduzi ya kuboresha na kuimarisha mbinu za uandaaji na usambazaji wa takwimu kwa wadau kwa kutumia fursa ya teknolojia ya kisasa zaidi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usamabazaji wa takwimu ili kupanua wigo wa matumizi ya takwimu kwa wadau mbalimbali.

Pamoja na hayo amesema kuwa NBS imekuwa inakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ambazo bado inaendelea kuzifanyiakazi ambazo amezitaja kuwa ni mahitaji makubwa ya takwimu kutoka kwa wadau ambayo yanapelekea uhitaji wa ongezeko la rasilimali zaidi za NBS.

Ametaja changamoto nyingine kuwa baadhi ya wazalishaji wa takwimu nchini kutofuata vigezo vya ubora vinavyotolewa na NBS pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya takwimu kwa baadhi ya watumiaji wa takwimu nchini.