September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBS kuzindua ripoti ya viashiria muhimu vya utafiti vya afya ya mzazi na mtoto,viashiria vya malaria 2022

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

OFISI ya Taifa ya Takwimu kesho inazindua Ripoti ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 huku ripoti hiyo ikitarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Lengo kuu la utafiti huo ni kupata taarifa za sasa za afya na takwimu zinazohusiana na masuala ya afya ili kusaidia kuboresha sera katika ajenda ya maendeleo ya kitaifa,kikanda na kimataifa.

Akizungumza  leo Februari 6,2023  kuhusu uzinduzi huo utakaofanyika katika Ofisi za Takwimu jijini Dodoma, Meneja wa Takwimu za Jamii,Sylvia Meku amesema pia uzinduzi huo umelenga kupata takwimu zitakazowezesha kupima viashiria vya malengo ya maendeleo ya kitaifa kama vile Dira ya maendeleo ya Tanzania 2025,Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.

Pia ripoti hiyo itawezesha kupima viashiria vya Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano(FYDP III 2021/22-2025/26),mpango wa maendeleo wa Zanzibar wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26,Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050(EAC 2050)Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063(ADA 2063)na Ajenda ya Kimataifa ya 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu(SDGs 2030)na kutathmini hatua iliyofikiwa katika kuboresha hali ya maisha ya watu hapa nchini.

Meku amesema,utafiti huo ulifanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS),Ofisi ya ya Mtakwimu Mkuu wa serikali Zanzibar (OCGS) na Wizara ya Afya Bara na Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Taasisi ya chakula na lishe Tanzania,mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria,Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika,Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Akizungumzia njia zilizotumika katika kufanya utafiti huo Meku amesema,utafiti huo ulifanyika kwa kutumia njia ya sampuli wakilishi kuwakilisha nchi nzima ambapo jumla ya maeneo ya kuhesabia watu 629 yalichaguliwa kuwakilisha maeneo mengine,

“Kati ya maeneo hayo,maeneo ya kuhesabia watu 211 yalikuwa ni ya Mijini na 418 ya Vijijini ambapo kwa kila eneo la kuhesabia watu,kaya 26 zilichaguliwa kitalaamu kuwezesha upatikanaji wa sampuli ya kaya wakilishi 16,354 nchini,”amesema Meku