January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBC kuanza kukopesha wachimbaji madini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KATIKA Kukuza uwekezaji wa sekta ya madini chini Benki ya Biashara ya Taifa NBC iko mbioni kuanzisha mfumo mpya wa ukopeshwaji wa mikopo kwa Wachimbani wa madini.

Mfumo huo utakaoondoa changamoto mbalimbali za uwekezaji kwa wachimbaji wadogo na wakubwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania 2022, Mkurungezi wa Biashara wa Benki ya NBC Elvis Ndunguru amesema hivi karibuni benki yao itaanzisha utaratibu wa kukopesha wachimbaji wadogo na wakubwa kwa kuweka dhamana ya madini yenyewe.

Ndunguru amesema, utaratibu huo utakuwa ni wa kwanza kuanzishwa na benki yao nchini ambao utampa fursa kwa mchimbaji wa madini kuweka dhamana ya madini yake na kuondoa usumbufu wa dhamana za mikopo kama awali.

“Hii ni mara ya kwanza kuanzishwa kwa utaratibu huu nchini na benki ya NBC ndiyo itakuwa ya kwanza nchini na itawapa fursa wachimbaji wadogo, wakubwa na wasambazaji kupata mkopo kwa urahisi,”

“Kufikia mwezi wa sita (June) tutakuwa tumeshaanza, mfumo umeshaandaliwa na hivi karibuni tutakuja kuelezea zaidi na namna mchimbaji atafaidika na mkopo kupitia madini anayoyachimba,” amesema Ndunguru.

Hata hivyo, Ndunguru amesema benki ya NBC imeondoa vikwanzo vya mikopo kwa wachimbaji wadogo na wakubwa ambapo kwa sasa wanapata mikopo kwa urahisi zaidi.

“Hata kama kuna mteja anahitaji kupata vifaa vya uchimbaji au magari kwa sasa kupitia benki ya NBC tumerahisisha upatikanaji wa mikopo kwa kuondoa vikwazo vyote ambapo awali ilikua inawafanya wachimbaji wasipate kwa uharaka,”

Kwa upande wa Mnufaika wa NBC,  Mwenyekiti wa Industrial Miners Tanzania Group Judith Sanga amesema benki ya NBC imekuwa na mchango mkubwa kwa sekta ya madini hususani kwa upande wao ambao wamerahisisha utaratibu wa mikopo kwa wachimbaji wa madini.

“Kiukweli Benki ya NBC imekuwa na mchango mkubwa sana, ni benki ya kwanza kutufikia sisi wachimbaji na utaratibu wao ni mzuri na wanakusiliza pale unapokuwa unahitaji msaada wako,”

“Wanachokitaka ni vile vigezo ambapo ni pampoja na leseni ya uchimbaji na mikopo unaipata kwa haraka na tunawashukuru sana,”

Benki ya Biashara ya Taifa NBC imewekeza zaidi katika sekta ya madini  nchini ili kuwasaidia wachimbaji na kuongeza pato la Taifa kwa nchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango akipata maelezo kutoka kwa mnufaika wa huduma za Benki ya NBC kupitia kitengo chao cha biashara, Mwenyekiti wa Industrial Miners Tanzania Group Judith Sanga wakati wa ufunguzi wa Mkutano Wa kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania 2022.