September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBAA yajidhatiti kuendana na mabadiliko ya Teknolojia

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea na mafunzo kwa wataalam kutoka vyuo na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha viwango vipya vya mabadiliko ya mtaala vinafuatwa katika utungaji wa mitihani, usahihishaji, na uhakiki na kuchagiza maendeleo ya kiuhasibu Nchini.

Ameyasema hayo leo Septemba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam MKURUGENZI wa Kurugenzi ya Elimu na Mafunzo wa NBAA, Peter Lyimo na kubainisha kuwa wataalam wanaoshiriki mafunzo haya wana jukumu kubwa la kuandaa mitihani inayolenga kuwapa wahitimu wa CPA ujuzi wa kutosha kwa ajili ya soko la ajira.

“Mafunzo hayo yanahusisha utungaji wa mitihani, usahihishaji, na uhakiki wa mitihani ili kuhakikisha viwango vipya vya mabadiliko ya mtaala vinafuatwa ili kuleta tija kwenye soko la ajira katika kuwajenga wahasibu na wakaguzi wenye ujuzi na weledi sahihi”. amesema Lyimo

Pia, wasahihishaji na wakaguzi wa mitihani wanapaswa kuzingatia malengo ya mitaala na matokeo ya ujifunzaji (learning outcomes), hasa tunapoingia kwenye masuala mapya ya sayansi na teknolojia kama vile sekta ya mafuta na gesi.

Hili linalenga kuwapa wahasibu ujuzi wa kusimamia kumbukumbu kwenye maeneo yanayoibuka kama “current issues.”

Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo wamesisitiza umuhimu wa kujifunza mbinu bora za kuandaa na kusahihisha mitihani ili kusaidia maendeleo ya nchi kwa kuzingatia mabadiliko ya mitaala.