Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amemuhakikishia aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo ambaye kwa sasa ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji kuwa amekabidhi Wizara katika mikono salama na kumuahidi kuwa yeye binafsi pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ni wanataaluma wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA hivyo pasipo shaka anaamini wanakwenda kutimiza matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimwa Samia Suluhu Hassan na watanzania kwa ujumla.
Sambamba na Makabidhiano ya Mawaziri hao yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba pia yalifanyika makabidhiano ya Ofisi baina Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula na kushuhudiwa na Menejimenti ya Wizara hiyo.
Nnauye amewapongeza Dkt. Kijaji na Dkt. Chaula kwa kazi nzuri walioifanya na kuwaahidi kuendeleza yale yote waliyokuwa wameanza kuyatekeleza katika harakati za kuboresha na kuendeleza Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA nchini.
Dkt. Kijaji ameishukuru Menejimenti ya Wizara hiyo kwa ushirikiano na uwajibikaji katika kipindi cha takribani miezi minne aliyohudumu katika Wizara hiyo na kuwasisitiza kufanyia kazi masuala yote yaliyokuwa katika hatua za utekelezaji kwa kuhakikisha yanafika mwisho mzuri unaotoa majibu na utatuzi uliokusudiwa.
Kwa upande wa Dkt. Jim Yonazi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema kuwa Dkt. Kijaji na Dkt. Chaula ni wadau muhimu wa Wizara hiyo, hivyo wataendelea kushirikiana, kushauriana na kupeana fursa mbalimbali kwa lengo la kujenga na kuboresha Sekta ambazo wameteuliwa kuzisimamia
Aidha, Dkt. Chaula ameishukuru timu ya Menejimenti ya Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa kwake ambapo pamoja na kuwa ni Daktari wa binadamu lakini amekuwa na weledi mkubwa wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA na ataendelea kuwa mdau mkubwa wa Wizara hiyo huku akiwausia watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii na kuacha alama.
More Stories
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara
Rais Samia aungwe mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia
Ushiriki wa Samia G20 wainufaisha Tanzania