January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

uwanja wa Nelson Mandela wa mjini Sumbawanga

Nani kuibuka mbabe kati ya Prison na Namungo leo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Rukwa

VIONGOZI mbalimbali mkoani Rukwa wamejitokeza kuwahamasisha wananchi mkoani humo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa mkoa huo unaochezwa leo katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga kati ya timu ya Tanzania Prison iliyohamishia makazi yake mjini Sumbawanga dhidi ya timu ya Namungo yenye makazi yake wilayani Ruangwa Mkoani Lindi.

Uwanja wa Nelson Mandela wa mjini Sumbawanga

Wakiongea katika nyakati mbalimbali pindi walipotembelea kuona maandalizi ya uwanja huo kwa ajili ya mechi hiyo wamesema kuwa hakika mechi hiyo itakuwa ni ya kihistoria katika mkoa wa Rukwa ambao hakuna timu hata moja ambayo imeshawahi kushiriki ligi kuu kwa Zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Akiongea kwa niaba ya kamati maalum ya mkoa inayoshughulika na kuilea timu katika Mkoa huo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Chrisant Mzindakaya aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo ambayo kwa sasa ndio timu ya nyumbani kwa watu wa mkoa huo.

“Timu hii ni mali yetu, si ya Magereza tena, kwa jina timu ya magereza lakini kwa vitendo ni timu ya mkoa huu wa Rukwa itakuwa hapa siku zote, tutakuwa nao siku zote ni na Namungo, Namungo haiwezi kuwashinda Magereza, lakini kubwa kuliko yote ni ninyi wananchi wa Sumbawanga hap ana vitongoji vyote mfike mshuhudie mchezo mzuri utaofanyika leo, tunaamini kiwango kilichowekwa cha kuingia hapa uwanjani ni cha kusaidia watu wengi muingie,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Rukwa Blasi Kiondo amewaalika wadau wote wa mpira wa ndani ya mkoa na wilaya zake pamoja na mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Songwe na Katavi kufika katika Uwanja wa Nelson Mandela kushuhudia mpamabano huo.

“Kiingilio chetu ni rahisi sana, tumeweka kiingilio cha Sh. 3000 kwa mzunguko wa uwanja mzima na tumeweka sh. 7000 kwa VIP, na nitangazie wanachi wote kuwa kuingia mapema ni vizuri zaidi kwa sababu kutakuwa na mechi chini ya umri wa miaka 17 itakayoanza saa tano mpaka saa sita mchana,” amesema.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Tanzania Prisons Jabu Adam Kifukwe amewahakikishia wadau wote wa mpira mkoani humo kuwa timu yao imejiandaa vyema kwa ajili ya mechi hiyo ya nyumbani na wasiwe na shaka juu ya wachezaji.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Justin Masejo amewahakikishia wananchi ulinzi na usalama kuanzia maandalizi ya mechi hiyo, kuanza kwa mechi hadi kumalizika kwake.