Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
UONGOZI wa timu ya Namungo FC ya Mkoani Lindi imewatahadharisha wapinzani wao Simba kuelekea mchezo wao wa kesho Julai 8 utakaochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa ambao utaambatana na sherehe za kukabidhiwa kombe lao ambalo wamelitwaa kwa msimu wa tatu mfululizo.
Simba ilitwaa ubingwa huo jijini Mbeya katika mchezo wao wa Juni 28 dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana lakini wakifanikiwa kufikisha pointi 79 ambazo zisingeweza kufikiwa na timu yoyote katika Ligi hata ikitokea wakapoteza mechi zao zote zilizosalia.
Wenyeji Namungo wamepanga kuingia katika mchezo huo huku wakitanga kulipa kisasi kwa Simba ambao waliwafun ga goli 3-2 katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Januari 29
Mbali na kutaka kulipa kisasi hicho lakini pia wanataka kuendeleza ushindi baada ya kuwafunga goli 1-0 Maafande wa JKT Tanzania katika mchezo wao uliopita katika uwanja huo.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Hitimana Thiery amesema, kwa sasa yupo kwenye maandalizi ya mwisho kabisa kabla ya kuwavaa wapinzani wao katika uwanja wao wa Majaliwa ambao wamepanga kuutumia kulipa kisasi na kuwatibulia sherehe yao.
Amesema, bado wana kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa Januari ambao wachezaji wake walionesha kiwango bora na cha kuvuti hivyo watahakikisha wanatumia mbinu walizozisoma kwa wapinzani wao kuwamaliza na kuchukua alama tatu.
“Baada ya juzi kupata ushindi dhidi ya JKT tulianza moja kwa moja maandalizi ya mechi yetu ya kesho dhidi ya Simba ambayo tumepanga kutumia madhaifu yao kuwaadhibu kama wao walivyofanya kwenye mchezo wetu wa mzuko wa kwanza ambao tulipoteza kwao,” amesema kocha huyo.
Mmoja wa wafanyabiashara karibu na uwanja wa Majaliwa ambaye pia ni shabiki wa timu hiyo, Kelvin Thomas ameuambia mtandao wa Timesmajira kuwa, wao kama mashabiki wamejipanga kujitokeza kwa wingi ili kuipa sapoti timu yao na kuhakikisha wanachukua alama tatu .
Amesema, wao kama mashabiki kikubwa wanachoomba kwa kocha Hitimana ni kuendelea kuwapa mbinu bora wachezaji wake ambazo zitawawezesha kuwafunga Simba na kubakiza ushindi.
“Katika msimamo wa Ligi timu yetu ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 59 lakini tunachokiomba ni kocha kuwapa mbinu bora za ushindi wachezaji ambazo zitatuwezesha kuongeza ponti na kugombea nagasi ya pili na Azam na Yanga zimetuacha kwa alama chache,” amesema Thomas.
More Stories
Naibu Waziri wa Fedha abariki ujio mpya wa Bahati Nasibu
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes