Na Mwandishi Wetu, Times Majira Online
YANGA wameamua kuachana na Mbelgiji Luc Eymael, aliyefundisha kwa miezi kadhaa. Ni baada ya mzungu huyo kukubali kutawaliwa na jazba mpaka akaongea maneno ya udhalilishaji na ubaguzi.
Hasira zikamjaa kichwani akajikuta akiwafananisha mashabiki wa Yanga na zile kelele za mnyama nyani. Kwa kweli alivuka mipaka na hakustahili kuendelea kuwa kocha mkuu wa Yanga.
Nashindwa kuwaweka katika kundi moja makocha wote wa kizungu kwa kuutumia msemo wa samaki mmoja akioza wengine wote wameoza pia. Vilabu vyetu bado vinayo nafasi kwa makocha wa kizungu.
Wanayo mengi mazuri kwa ajili ya Taifa Stars, Zanzibar Heroes, Yanga, Simba, Azam na vilabu vingine vingi tu. Kwanza kabisa wanakuja kufanya kazi wakitaka kutunza heshima ya wasifu wao binafsi.
Pili wanakuja kwa nia ya kukuza viwango vya uchezaji wa vilabu vyetu, wanakuja kwa nia ya kuukuza muelekeo mzima wa timu.
Hii sababu ya pili ni ya muhimu siku zote. Ni hiyo ambayo inawagombanisha na vilabu vinavyowapa ajira, kwani wao hawakubaliani na mazoea yetu ya kila siku ya kiuendeshaji.
Mara nyingi kocha wa kizungu anapoanzishiwa majungu, ni kwamba anakuwa kashikilia msimamo wake wa kimaadili na wanaomzunguka wanashikilia uamuzi wa kimazoea.
Makocha wazalendo siku zote huwa wanashindwa kuja na maoni mapya yenye kufuata maadili ya ufundishaji, pengine wakiogopa nguvu ya ushawishi ya mashabiki na wanachama wa timu.
Wanajikuta wakikubaliana hata na hoja zisizo na mashiko kwenye maadili ya kisoka, ilimradi tu ajira zao ziendelee kuwepo. Wanakuwa ni makocha ‘wenzetu’, wasioweza kujiweka katika upande wa usiokubaliana na masuala ya ubabaishaji.
Kocha wa kizungu kwanza kafundisha kwao miaka kadhaa kama kocha msaidizi, baadae akapata ajira katika vilabu viwili vitatu vya Afrika kabla hajaja kuifundisha Simba au Yanga.
Huko alikopita amefanya kazi kwa kuheshimu miiko ya soka, na wasifu uliomuuza mpaka akaonwa na viongozi wa timu zetu umejengwa katika kuheshimu taratibu za kimataifa.
Kocha mkuu wa Simba kaitazama timu kwa kina tangu apawe ajira, kaona mengi tu kwa mtazamo wa kitaalam. Inasemekana katika kundi lote la wachezaji aliowakuta amependekeza wachezaji sita tu ndio wabakishwe na wengine watafute timu.
Kocha huyo ametazama ushindani wa kweli wa mechi za kimataifa jinsi ulivyo halafu akalinganisha na kile anachokiona mazoezini na siku za mechi.
Ameuona upungufu mwingi wa kufanyiwa kazi iwapo kweli Simba inataka iwe ni timu inayofika mbali katika michuano ya bara la Afrika.
Pengine makocha wazalendo wasingekuwa na ujasiri wa kuwaambia viongozi kwamba lipo kundi kubwa la wachezaji wenye viwango vya humu humu katika ushiriki wa mechi za ligi kuu pekee.
Pengine makocha wazalendo peke yao wangeandaa ripoti iliyojaa huruma kwa ajira za wanasoka vijana wa Kitanzania. Kocha wa kizungu akiliona embe analiita embe, akiliona chungwa analiita chungwa, hapindishi maneno.
Uwepo wao unasaidia sana katika kuukuza mtazamo wa kiushindani miongoni mwa wanasoka wetu. Wao kuwa wakweli ni jambo lenye manufaa kwa wanasoka wetu ambao uwezo wao wa kiushindani ni mdogo kimataifa.
Vituo vingi vya kukuzia vipaji vya wanasoka vya Afrika Magharibi vinasimamiwa kwa kufuata taratibu zile zile za weledi wa soka. Ni ukweli kabisa Luc Eymael amevuka mipaka kwa kuamua kutumia lugha ya ubaguzi wa rangi.
Lakini Eymael ni mzungu mmoja tu na pesa ina nguvu ya kuwaajiri makocha wazungu wengine wenye akili nzuri tofauti na yeye. Eymael mmoja asiyejielewa vyema hawezi kuufanya uwezo wa kuishi vizuri na watu alionao Marcio Maximo ukawa hauna maana.
Eymael mmoja na hasira zake za haraka hawezi kuwa ndio kigezo cha mataifa ya Afrika Magharibi kutoajiri makocha wakubwa kutoka Ulaya. Misri inae Hassan Shehata, kocha mzalendo mwenye historia ya kubeba kombe la AFCON mara tatu mfululizo.
Mrithi wake akawa ni Muargentina Hector Cuper, haikuwa na maana kwamba ukiondoa Shehata hakuna kocha mwingine mzalendo wa Misri mwenye uwezo mkubwa.
Misri walitaka kupata changamoto mpya ya ufundishaji, walitaka kupata uzoefu mpya.
Hivyo alichofanya Luc Eymael kwa wadau wa soka kwa ujumla wao, ni jambo lenye kukera lakini haliwezi kuwa ndio kigezo cha vilabu vyetu kuamini kwamba makocha wote wa kigeni hawana jipya.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
Miaka 63 ya Uhuru na rekodi treni ya SGR